#HABARI: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa wafanyabiashara wadogo (machinga) wa eneo la Kariakoo kuhakikisha wanafungua njia zinazozunguka soko hilo ili kuruhusu magari na shughuli nyingine za kibiashara kufanyika kwa ufanisi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 30, 2025, Chalamila amesema hatua hiyo ni muhimu kuelekea uzinduzi wa soko jipya la Kariakoo ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98, na kwamba ni lazima maandalizi yawe yamekamilika ifikapo muda wa uzinduzi rasmi.
“Natoa muda wa wiki mbili ili uongozi wa Kariakoo na wafanyabiashara ndogondogo wawaeleze kuhusu dhamira ya Serikali na namna ya kufungua njia ili kila mmoja abebe mzigo huu wa kufanikisha shughuli hii. Tusipofanya hivyo, tutajikuta tunabaki na soko lisilo na tija licha ya uwekezaji mkubwa uliokwisha kufanyika,” amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa Serikali haitakubali kuona uwekezaji mkubwa uliofanyika katika ujenzi wa soko hilo ukikwamishwa na baadhi ya watu kushikilia maeneo kiholela. Aidha, amewataka viongozi wa wafanyabiashara hao kutoa elimu na ushawishi kwa wanachama wao ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa amani na ufanisi.
Soko jipya la Kariakoo linatajwa kuwa la kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki, likitarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara jijini Dar es Salaam na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.