#HABARI: Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe

#HABARI: Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, umetekeleza kwa vitendo dhana ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia sekta za Uzalishaji.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa hosteli ya wasichana na kumbi mbili za mihadhara kwenye Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kampasi ya Mpwapwa, mkoani Dodoma ambapo mbali na kuupongeza uongozi wa Wilaya ya chuo hicho kwa kukamilisha ujenzi wa majengo hayo kwa viwango stahiki amefurahishwa na namna wanafunzi wa chuo hicho walivyoandaliwa kuwa wataalam wazuri wa sekta ya Mifugo.

Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa mbali na ujenzi wa majengo hayo na ukarabati wa kampasi mbalimbali za Wakala hiyo zilizogharimu Bil.1.9, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati miundombinu mingine ya Wakala hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa shilingi milioni 168 za ukarabati wa mabweni mawili ya kampasi ya Temeke.

Mbali na Ujenzi wa Majengo ya Wakala hiyo yaliyozinduliwa, ambao umegharimu takribani kiasi cha shilingi Bil. 1.6, Wakala hiyo imeanza ujenzi wa Kampasi nyingine mkoani Songwe itakayogharimu shilingi Bil. 1.2 hadi kukamilika kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *