#HABARI: Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, umemkamata Bw

#HABARI: Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, umemkamata Bw. David Mhame, mkazi wa Yombo Kilakala Dar es Salaam na kumpeleka Kituo cha Polisi Salender Bridge kwa tuhuma za kutapeli wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kwa huduma mbalimbali.

Bw. Mhame amekamatwa baada ya kupokea taarifa za kutaka kumtapeli Bi. Fatuma Mohamed, mkazi wa Kigogo kiasi cha Shilingi Mil. 1.2 ili aweze kumsaidia, kuchukua mwili wa ndugu yake uliopo hospitalini hapo.

Kwa mujibu wa Bi. Fatuma mtuhumiwa alijumuika katika kikao cha ndugu na kujifanya ni sehemu ya familia na kuwashauri kutafuta kiasi hicho cha fedha ili waweze kuchukua mwili kwa ajili ya mazishi lakini baadaye walimshtukia na kuanza kumhoji na walipobaini hatoi taarifa zinazoeleweka walitoa taarifa kwa uongozi wa hospitali hiyo na hatimaye kumkamata.

Bi. Fatuma ameongeza kuwa awali mtuhumiwa alimtapeli kiasi cha Shilingi laki tatu mwezi Januari, 2025 walipokuwa katika taratibu za kuchukua mwili Hospitali ya Taifa Muhimbili-Upanga na walipojaribu kumtafuta hawakufanikiwa kumpata.

Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili unaendelea kuwakumbusha wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo kutotoa fedha taslimu (cash) kwa mtu yeyote kwani malipo ya huduma zote zinafanywa kupitia namba ya kumbukumbu ya malipo ya Serikali (control number).

#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania.

#Follow @radioonetanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *