Takribani watu 14 wapoteza maisha, 750 wajeruhiwa kwa mlipuko mkubwa katika bandari kuu ya Iran

Moshi mzito

Chanzo cha picha, EPA

Takribani watu 14
wamepoteza maisha na 750 kujeruhiwa katika mlipuko mkubwa katika bandari moja
muhimu ya Iran, mamlaka zilisema.

Mlipuko huo
ulitokea katika eneo la Shahid Rajaee, bandari kubwa zaidi ya kibiashara nchini
humo, karibu na mji wa kusini wa Bandar Abbas Jumamosi asubuhi.

Iliharibu madirisha
na kuezua paa za majengo ya karibu na kuharibu magari. Wakazi waliripoti kuhisi athari
za mlipuko huo ulio umbali wa kilomita 50 (maili 31).

Video
zilizothibitishwa na BBC zinaonesha moto ukizidi kuwaka kabla ya mlipuko
mkubwa, huku watu wakikimbia mlipuko huo na wengine wakiwa wamelala wakiwa
wamejeruhiwa kwenye barabara zilizozingirwa na moshi mzito.

“Ghala lote
lilikuwa limejaa moshi, vumbi na majivu. Sikumbuki ikiwa nilienda chini ya meza
au nilirushwa pale na mlipuko huo,” mtu mmoja aliyekuwa katika eneo hilo
aliiambia runinga ya serikali.

Picha za angani
zilionesha takribani maeneo matatu yakiwaka moto na waziri wa mambo ya ndani wa
Iran baadaye alithibitisha kuwa moto huo ulikuwa ukisambaa kutoka kontena moja
hadi jingine. Shule na ofisi katika eneo hilo zimeamriwa kusalia kufungwa siku
ya Jumapili.

Maafisa wa forodha baadaye walitoa taarifa
iliyoripotiwa na Televisheni ya taifa ya Iran wakisema kuwa huenda mlipuko huo
ulitokana na moto ambao ulizuka katika ghala la hazmat la kuhifadhi vifaa vya
kemikali.

Katika sasisho la
baadaye Ambrey alinukuu Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Majanga la Iran
likisema maafisa hapo awali walitoa onyo kwa bandari ya Shahid Rajaee kuhusu
uhifadhi salama wa kemikali.