Chanzo cha picha, BBC News
Maelezo ya picha, Mchoro: Jaribio litazunguka Dunia kwa saa tatu kabla ya kurejea Duniani na kuanguka kwenye pwani ya Ureno.
Maelezo kuhusu taarifa
- Author, Pallab Ghosh
- Nafasi, Ripota wa sayansi
- Twitter, @BBCPallab
-
26 Aprili 2025, 10:01 EAT
Imeboreshwa Dakika 26 zilizopita
Nyama, viazi na mapochopocho ya wanaanga huenda yakaanza kukuzwa kutoka kwa seli ya anga iwapo jaribio ambalo limeanza wiki hii litakuwa na ufanisi.
Kulingana na shirika la anga la Ulaya(ESA) ni mpango unaotathmini ukuzaji wa chakula kwa maabara katika miale ya mwanga katika mzingo wa dunia na sayari zingine.
ESA inafadhili utafiti unaochunguza njia mbadala za kupunguza gharama ya lishe ya wanaanga ambayo hugharimu takriban paundi 20,000 kila siku.
Kikundi kinachohusika kimeeleza kuwa awamu ya kwanza ni kubuni eneo la kukuza chakula katika stesheni ya kimataifa ya anga ndani ya miaka miwili.
Chakula kilichokuzwa katika maabara kitasaidia pakubwa mpango wa NASA wa kuhakikisha kuna maisha na uhai wa binadamu katika anga za mbali, anadai Dkt Aqeel Shamsul, ambaye ni mkurugenzi na muanzilishi wa shirika la Bedford-based Frontier Space ambalo linabuni mchakato huu kwa ushirikiano na watafiti kutoka kwa Chuo kikuu cha Imperial, mjini London.
”Ndoto yetu ni kuwa na viwanda katika mzingo wa dunia na katika mwezi,” anaiambia BBC
”Tunapaswa kujenga viwanda nje ya dunia iwapi tunapendelea miundo msingi ambao utawezesha binadamu kuishi na kufanya kazi katika anga za mbali”.
Pia unaweza kusoma:
Chanzo cha picha, NASA
Maelezo ya picha, Wanaanga wanafurahia wakila huku wakielea, lakini chakula kilichokaushwa hakifurahishi nafsi
Chakula kilichokuzwa katika maabara kinajumuisha virutubisho kama vile proteni, mafuta na kabohaidreti katika bomba la maabara nakishakusindikwa kikae na kiwe na ladha kama chakula cha kawaida.
Kuku aliyekuzwa katika maabara tayari anauzwa katika soko la Marekani na Singapore na nyama iliyokuzwa kwa njia hiyo pia inatarajiwa kuidhinishwa Uingereza na Israel.
Duniani kuna madai kuwa kuna umuhimu wa mazingira kwa teknolojia ukilinganisha na ukuzaji wa chakula kiasili kama vile kutotumia ardhi kubwa kukuza chakula na pia kupunguza gesi inayofuka katika chumba cha kioo cha kuhifadhi mimea.
Lakini katika anga za mbali shinikizo la kukuza chakula ni kwa ajili ya kupunguza gharama.
NASA, mashirika mengine ya anga na makampuni ya sekta ya kibinafsi yanapanga kuwa na uwepo wa muda mrefu kwenye Mwezi, katika vituo vya anga vinavyozunguka na labda siku moja kwenye sayari ya Mars.
Hiyo itamaanisha kupeleka chakula kwa makumi na hatimaye mamia ya wanaanga wanaoishi na kufanya kazi angani – jambo ambalo lingekuwa ghali sana ikiwa lingetumwa na roketi, kulingana na Dkt Shamsul.
Kukuza chakula angani kunaweza kuwa na maana zaidi, anapendekeza.
“Tunaweza kuanza tu na viazi vilivyopondwa vilivyoimarishwa kwa protini hadi kwenye vyakula ngumu zaidi ambavyo tunaweza kuweka pamoja angani,” ananiambia.
“Lakini baada ya muda mrefu tunaweza kuweka viambato vilivyokuzwa kwenye maabara kwenye kichapishi cha 3D na kuchapisha chochote unachotaka kwenye kituo cha angani, kama vile nyama!”
Maelezo ya picha, Nyama iliyokuzwa kwa maabara inaweza kubuniwa duniani lakini je inaweza kukuzwa katika anga za mbali?
Yale yaliyokuwa yakionekana kama ndoto za kisayansi katika filamu kama Star Trek ambapo mashine huchukua nishati pekee na kuitengeneza kuwa chakula au kinywaji sasa yanakaribia kuwa uhalisia.
Dkt. Shamsul anasema, “Hii si sayansi ya kubuni tena.”
Katika Kituo cha Bezos cha Protini Endelevu, kilichopo Chuo cha Imperial, London, alinionyesha kifaa kinachoitwa bioreactor—mashine ya kisasa inayofanya kazi ya uchachushaji kwa usahihi mkubwa.
Ndani yake kulikuwa na mchanganyiko wenye rangi ya udongo ukichemka polepole ndani ya bomba la majaribio.
Mchakato huu unaitwa precision fermentation — aina ya uchachushaji unaofanana na ule wa kutengeneza bia, lakini tofauti kubwa ni kwamba viumbe vinavyotumika vimetengenezwa kwa teknolojia ya vinasaba.
Kwa mfano, katika majaribio haya, jeni limepandikizwa kwenye hamira ili iweze kuzalisha vitamini za ziada.
Lakini uwezo wa teknolojia hii hauishii hapo.
Kwa mujibu wa Dkt. Rodrigo Ledesma-Amaro, mkurugenzi wa kituo hicho, “Tunaweza kutengeneza kila kipengele muhimu cha chakula—protini, mafuta, wanga, na hata nyuzinyuzi.”
Kwa kutumia viambato hivyo, anaeleza, vinaweza kuchanganywa kwa ustadi ili kuunda aina mbalimbali za chakula. “Kwa teknolojia hii, hatuzungumzii tena tu kuhusu chakula cha baadaye; tunakikaribisha mezani leo.”
Maelezo ya picha, Chakula kilicho na rangi ya udongo kinakuzwa kwa mashine ambayo imesafirishwa hadi anga za mbali
Toleo dogo, la kisasa na rahisi la bioreactor sasa limepelekwa angani kwa kutumia roketi ya SpaceX Falcon 9, chini ya mradi wa Shirika la Anga la Ulaya (ESA).
Ingawa sayansi imethibitisha kuwa chakula kinaweza kuzalishwa duniani kupitia seli, bado haijafahamika iwapo mchakato huo unaweza kufanikiwa katika mazingira ya uzito hafifu na mionzi mikali ya anga za juu.
Madaktari Rodrigo Ledesma-Amaro na Shamsul wamechukua hatua ya kihistoria: wamepeleka kiasi kidogo cha mchanganyiko wa hamira katika obiti ya dunia kupitia satelaiti ndogo ndani ya Phoenix chombo cha kwanza cha kibiashara cha Ulaya kinachoweza kurudi salama duniani.
Kulingana na mpango, satelaiti hiyo itazunguka Dunia kwa saa tatu kisha kuanguka karibu na pwani ya Ureno.
Kifaa hicho kitapokewa na kikosi maalum cha uokoaji na kurejeshwa maabara mjini London kwa uchambuzi wa kina.
Haya yatafanyika shughuli hiyo ikipata ufanisi.
Matokeo ya jaribio hili yatatumika kuunda bioreactor kubwa na yenye uwezo zaidi, ambayo wanasayansi wanapanga kuituma angani mwaka ujao, anasema Dkt. Ledesma-Amaro.
Lakini changamoto haiko kwenye teknolojia pekee, bali pia kwenye ladha na mvuto wa chakula hicho.
Mchanganyiko wenye rangi ya tofaa ambao hukauka na kuwa unga, hauna mvuto wowote kwa jicho wala hamu ya kula unaweza hata kuonekana duni kuliko vyakula vya kukaushwa wanaanga wanavyolazimika kutumia kwa sasa.
Ndipo kipaji cha Jakub Radzikowski, mpishi mkuu na mbunifu wa elimu ya upishi katika Chuo cha Imperial, kinapohitajika.
Yeye amepewa jukumu maalum: kuibadilisha kemia kuwa mapishi ya kuvutia.
Kazi yake ni kugeuza unga wa kisayansi kuwa mlo unaovutia hisia na kufurahisha ladha kuleta mapinduzi ya upishi wa anga za juu.
Chanzo cha picha, Kevin Church
Maelezo ya picha, Mpishi wa Chuo Kikuu cha Imperial ana jukumu la kubadilisha kemia kuwa chakula kitamu
Ingawa bado hajapata idhini rasmi ya kutumia viambato vilivyozalishwa maabara kwa ajili ya mapishi ya watu, Jakub Radzikowski haoneshi kusita.
Akiganga yajayo, ameanza majaribio kwa kutumia mbadala wa asili wanga na protini zinazotokana na uyoga pori kuunda mapishi ya kisayansi yanayoelekea kubadili sura ya chakula cha anga za juu.
Anasema, mara tu atakapopata kibali cha kutumia viambato vilivyotengenezwa maabara, milango itafunguka kwa mapishi ya kila aina.
“Lengo letu ni kuunda vyakula vinavyoamsha kumbukumbu na faraja kwa wanaanga kutoka pembe mbalimbali za dunia,” anasema kwa msisitizo.
“Tutakuwa na uwezo wa kutengeneza mapishi ya Kifaransa, Kichina, Kihindi tutapata ladha yoyote ile, hata angani.”
Leo hii, Jakub anajaribu mapishi mapya: kamati zenye viungo kali na mchuzi wa kuzitumbukiza.
Ananiambia kuwa ninaweza kuonja, lakini heshima ya kuwa mtaalamu mkuu wa ladha imepewa mtu maalum Helen Sharman, mwanaanga wa kwanza wa Uingereza, ambaye pia ni mtaalamu wa kemia mwenye shahada ya uzamifu.
Ni mchanganyiko wa sayansi, ubunifu na urithi wa ladha kazi ya mpishi huyu bingwa inaufungua ukurasa mpya wa kile chakula kinaweza kuwa, hata nje ya mipaka ya Dunia.
Chanzo cha picha, Kevin Church/BBC News
Maelezo ya picha, Mwanaanga wa kwanza wa Uingereza, Helen Sharman, na mimi tunaonja tunajaribu kile ambacho kinaweza kuwa chakula cha anga cha siku zijazo
Tulionja pamoja kaimati zilizokuwa zinatoa mvuke.
Maoni yangu yalikuwa ya haraka na dhahiri: “Zina ladha tamu kupita maelezo!”
Lakini ilikuwa ni tathmini ya kitaalamu ya Dkt. Helen Sharman iliyoonyesha uzito wa kile kilichokuwa mbele yetu: “Unapigwa na ladha kali ya kuvutia. Ni tamu kweli, na unataka tu uendelee kula,” alisema kwa furaha.
Akaongeza kwa kutafakari, “Ningetamani sana kupata chakula kama hiki nilipokuwa angani. Tulikuwa na vyakula vyenye maisha marefu—makopo, pakiti za kukaushwa, mirija ya chakula. Vilitosha kwa lishe, lakini havikuwa na ladha ya kuvutia.”
Hata hivyo, alichosisitiza zaidi kilikuwa ni mchango wa kisayansi wa chakula kinachozalishwa maabara.
Kwa mujibu wa Dkt. Sharman, mbinu hii inaweza kuleta mapinduzi katika lishe ya wanaanga si tu kwa kuboresha afya zao, bali pia kwa kupunguza gharama za safari na makazi ya muda mrefu nje ya Dunia.
Utafiti katika Kituo cha Anga cha Kimataifa (ISS) unaonyesha kuwa miili ya wanaanga hubadilika wanapokuwa kwenye anga kwa muda mrefu: homoni hubadilika, viwango vya madini ya chuma hupungua, na mifupa hupoteza kalisi.
Ingawa sasa hutumia virutubisho kukabiliana na hali hiyo, Dkt. Sharman anaeleza kuwa chakula kilichotengenezwa maabara kinaweza kuundwa mahsusi kikiwa na virutubishi hivyo tayari vimejumuishwa.
“Wanaanga hupungua uzito kwa sababu ya upungufu wa hamu ya kula – ukosefu wa utofauti na mvuto katika mlo wao wa kila siku,” anaeleza.
“Kwa hiyo, huenda wakapokea kwa mikono miwili chakula halisi kilichopikwa kwa ubunifu kinachokaribisha hisia za ladha, ukaribu, na afya njema.”