Kuzuiliwa kwa Riek Machar kunahitimisha makubaliano ya kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe – SPLM/IO

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Riek Machar

Kuzuiliwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar kumevunja mkataba wa amani wa 2018 uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano nchini humo, chama chake kimesema.

Msafara wenye silaha ukiongozwa na maafisa wakuu wa usalama, akiwemo waziri wa ulinzi, uliingia katika makazi ya Machar katika mji mkuu, wa Juba, na kuwanyang’anya silaha walinzi wake siku ya Jumatano, kilisema chama cha Sudan People’s Liberation Movement In Opposition (SPLM/IO).

Machar alizuiliwa pamoja na mkewe Angelina Teny, ambaye ni waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo, chama hicho kiliongeza.

“Kukamatwa na kuzuiliwa kwa Dkt. Riek Machar kunasababisha makubaliano ya [amani] kuporomoka,” alisema naibu kiongozi wa SPLM/IO Oyet Nathaniel Pierino.

Serikali bado haijatoa tamko juu ya kuripotiwa kukamatwa kwa Machar nyumbani.

Akiwahutubia viongozi wa kidini siku ya Jumatano, Rais Salva Kiir alisema “hatawahi kuirejesha nchi vitani”.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukionya kuwa Sudan Kusini iko kwenye ukingo wa kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kufuatia kuongezeka kwa mzozo kati ya Machar na rais ambao umeendelea kwa wiki kadhaa.

Viongozi hao wawili walikubaliana mnamo Agosti 2018 kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoua karibu watu 400,000.

Lakini katika kipindi cha miaka saba iliyopita uhusiano wao umezidi kuwa mbaya huku kukiwa na mivutano ya kikabila na ghasia za hapa na pale.