Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Rais Ramaphosa na mwenzake wa Ukraine Zelensky
Maelezo kuhusu taarifa
- Author, Farouk Chothia
- Nafasi, BBC News
-
Dakika 4 zilizopita
Ziara ya kihistoria ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, nchini Afrika Kusini inaashiria ukurasa mpya katika uhusiano kati ya mataifa haya mawili, ambao hapo awali ulikuwa na misuguano.
Ziara hii imeonekana kama hatua muhimu ya kidiplomasia kwa Zelensky katika juhudi zake za kupunguza ushawishi mkubwa na unaokua wa Urusi barani Afrika.
“Bila shaka Urusi haitafurahishwa na ziara hii, lakini nina shaka kama inaweza kuchukua hatua yoyote ya maana dhidi yake,” anasema Steven Gruzd kutoka Taasisi ya Mahusiano ya Kimataifa ya Afrika Kusini.
Tangu achaguliwe mwaka 2019, Zelensky hajawahi kufanya ziara rasmi barani Afrika isipokuwa kupitia kwa muda mfupi Cape Verde mwaka 2023 alipokuwa safarini kuelekea Argentina.
Ukraine ilianza kutambua umuhimu wa bara la Afrika katika diplomasia ya kimataifa baada ya nchi nyingi zikiwemo zile zenye ushawishi kama Afrika Kusini kushindwa kulaani uvamizi wa Urusi mwaka 2022.
“Kwa muda mrefu, Ukraine haikutoa kipaumbele kwa Afrika katika sera zake za kigeni. Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, imebadilisha mkakati huo kwa kuongeza idadi ya balozi zake kutoka 10 hadi 20,” Bw. Gruzd aliiambia BBC.
Hata hivyo, Ukraine inaingia katika uwanja wenye ushindani mkubwa wa kimaslahi, ambapo mataifa kama Urusi, China, Uturuki na Falme za Kiarabu yamekuwa yakiwekeza kwa nguvu katika mahusiano ya kisiasa na kiuchumi barani Afrika.
Ziara hii inakuja wakati mgumu kwa Ukraine, hasa ikizingatiwa kuwa uhusiano wake na Marekani taifa linaloongoza kwa kutoa misaada ya kijeshi umedhoofika tangu Rais Donald Trump aingie madarakani mwezi Januari.
Trump amesitisha misaada ya kijeshi kwa Ukraine, amemshutumu Zelensky kwa kuwa “dikteta,” na ameilaumu nchi hiyo kwa kusababisha vita vinavyoendelea.
“Ukraine inahitaji kupata uhalali wa kimataifa kwa kila njia iwezayo siyo tu kutoka Ulaya. Vita havishindwi tu kwa silaha vitani, bali pia kwa kushinda mioyo na fikra za watu duniani,” anasema Profesa Siphamandla Zondi kutoka Chuo Kikuu cha Johannesburg.
Kwa upande mwingine, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, pia anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa utawala wa Trump, jambo linalofanya ziara hii kuwa na uzito mkubwa kisiasa kwa pande zote mbili.
“Diplomasia imebadilika kabisa chini ya utawala wa sasa wa Marekani,” anasema Gruzd, akihitimisha kwa kusema: “Kila taifa sasa linatafuta marafiki wapya.”
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Vita vimesababisha hasara kubwa
Rais Cyril Ramaphosa anatazama ziara ya Rais Volodymyr Zelensky kama fursa ya kuimarisha nafasi yake kama mpatanishi wa kimataifa, akieleza kuwa mazungumzo yao yataangazia juhudi za pamoja za kutafuta suluhu ya kudumu ya amani.
Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alithibitisha kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Rais Vladimir Putin kabla ya kuwasili kwa Zelensky.
“Tulidhibitisha uimara wa uhusiano wa pande mbili kati ya mataifa yetu,” Ramaphosa aliandika kwenye mtandao wa X, akiongeza kuwa wamekubaliana kushirikiana katika mchakato wa kuumaliza mzozo wa kivita kati ya Urusi na Ukraine.
Hili si jaribio lake la kwanza.
Mwaka wa 2023, Ramaphosa aliongoza ujumbe wa viongozi wa Afrika kwenda Kyiv na Moscow kwa lengo la kusuluhisha mzozo huo.
Hata hivyo, juhudi hizo zilifanyika wakati ambapo Afrika Kusini ilikuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa utawala wa Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden.
Marekani ilitilia shaka msimamo wa Pretoria wa kutoegemea upande wowote, hasa baada ya kushiriki mazoezi ya kijeshi na Urusi pamoja na China.
Hali ilizidi kuwa tete baada ya balozi wa Marekani kudai kuwa Afrika Kusini ilisafirisha silaha na risasi kwenda Urusi.
Ramaphosa alijibu kwa kuanzisha uchunguzi huru ulioongozwa na jaji, ambao hatimaye haukupata ushahidi wa kuunga mkono madai hayo.
Hata hivyo, uhusiano kati ya Pretoria na Washington uliendelea kuwa na wasiwasi.
Kwa upande mwingine, uhusiano wa Ramaphosa na Urusi haujakuwa na madhara ya moja kwa moja kwa Donald Trump, ambaye anaonekana kuwa na urafiki wa karibu na Putin.
Trump amekuwa akimhimiza Zelensky kufikia makubaliano na Urusi.
Hata hivyo, uhusiano wa Trump na Afrika Kusini umeporomoka sana kufuatia hatua ya serikali ya Ramaphosa kufungua kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), na pia kutokana na shutuma za Trump kuhusu kile anachokiita “unyanyasaji wa Wazungu waafrika-Afrikaneers”, madai ambayo serikali ya Afrika Kusini imeyakanusha vikali.
Kwa mujibu wa Profesa Siphamandla Zondi, Afrika Kusini itahitaji kuwa makini ili mazungumzo ya Ramaphosa na Zelensky yasilete madhara kwa juhudi zake za kurejesha uhusiano mzuri na utawala wa Trump.
“Afrika Kusini italazimika kufafanua wazi kwamba inachangia katika juhudi za kimataifa za kujenga amani, na haijajitwika jukumu la kushindana na Marekani,” alisema.
Aidha, Profesa Zondi alibainisha kuwa Ramaphosa anaweza kutumia ziara hiyo kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Ukraine, hasa ikizingatiwa kuwa Afrika Kusini inakumbwa na mdororo wa uchumi, ukuaji duni wa maendeleo, na uhaba wa ajira nchini humo.
“Biashara ya kiwango chochote ni muhimu kwa Afrika Kusini. Na uhusiano wa karibu unaweza kuwa msaada kwa Ukraine kupanua ushawishi wake barani Afrika,” alieleza.
Kwa mtazamo wake, Afrika Kusini inaweza kuwa lango la Ukraine kuingia Afrika, ikizingatia uwezo wake katika miundombinu ya bandari na mifumo ya kifedha.
Iwapo uhusiano huo utaimarika, basi huenda ukafungua ukurasa mpya wa uhusiano kati ya Ukraine na bara la Afrika lakini si kwa gharama ya Urusi.
“Urusi na Ukraine ndizo wasambazaji wakuu wa nafaka kwa Afrika. Bara hili linawahitaji wote. Si haki kulazimishwa kuchagua upande mmoja,” Profesa Zondi alihitimisha.
Mada zinazofanana:
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi