Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Massad Boulos anasema ushuru wa Marekani na kupunguzwa kwa misaada unalenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji
Maelezo kuhusu taarifa
- Author, Wycliffe Muia & Rob Young
- Nafasi, BBC News
-
Dakika 28 zilizopita
Mshauri Mkuu wa Marekani barani Afrika Massad Boulos amesema kuwa Rais Donald Trump anaithamini Afrika, licha ya kutangaza kupunguzwa kwa misaada ambayo imesababisha maafa makubwa ya kibinadamu katika bara zima.
Trump alitangaza kusitishwa kwa msaada huo mapema mwaka huu mara alipoingia madarakani kwa kuzingatia sera yake “Marekani Kwanza”.
Ushuru wake wa hivi karibuni umeibua hofu ya kumalizika kwa makubaliano ya kibiashara kati ya Marekani na Afrika yaliyokusudiwa kukuza ukuaji wa kiuchumi.
Lakini Bw Boulos aliambia BBC kwamba Afrika ni “muhimu sana” kwa Trump na kupuuza madai kwamba Marekani ilikuwa na mpango wa kufunga baadhi ya balozi zake barani humo.
“Anathamini sana Afrika na watu wake,” Bw Boulos aliongeza.
Kupunguzwa kwa misaada hiyo kumeathiri mipango ya afya barani Afrika, ikijumuisha usafirishaji wa vifaa muhimu vya matibabu, pamoja na dawa za kukabiliana na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Mataifa manane – sita kati ya hizo za Kiafrika, zikiwa ni pamoja naNigeria, Kenya na Lesotho – huenda zikaishiwa na dawa za VVU kufuatia hatua ya Marekani kusitisha misaada ya kigeni, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya.
Kuna hofu kwamba takriban Waafrika zaidi milioni sita wanaweza kutumbukia katika umaskini uliokithiri mwaka ujao kufuatia kupunguzwa kwa misaada, kulingana na Taasisi ya Mafunzo yaUsalama.
Mapema mwezi huu, watu wanane, wakiwemo watoto watano, walifariki baada ya kutembea kwa saa kadhaa kutafuta tiba ya maradhi ya kipindupindu nchini Sudan Kusini baada ya hatua ya utawala wa Trump ya kusitisha misaada kusababisha kliniki za afya za eneo hilo kufungwa, Shirika la Kimataifa la misaada la Save the Children liliripoti.
Lakini Bw Boulos alisema vifo hivyo vilivyoripotiwa haviwezi kuhusishwa moja kwa moja na kupunguzwa kwa misaada ya Marekani na kusema kwamba hatua madhubuti zinahitajika ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo.
“Ni muhimu [kwa Marekani] kukagua baadhi ya programu hizi kwauwazi,” Bw Boulos alisema.
“Tunapaswa kuhakikisha [fedha za misaada] zinawafikia walengwa na ufanisi wake uweze kuonekana,” aliongeza.
Bw Boulos, alisema kampuni kadhaa za Marekani zimeonyesha nia ya kunyonya madini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kufuatia safari yake ya hivi majuzi katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali huko Afrika ya kati.
DR Congo, ina hifadhi kubwa za raslimali asili kama lithium ambayo ni muhimu kwa utengenezaji wa betri na magari ya umeme, imekuwa ikipambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wameteka maeneo makubwa mwaka huu.
Rais wa Kongo Félix Tshisekedi anaamini kuhusika kwa Marekani katika uchimbaji wa madini hayo kunaweza kusaidia kutuliza ghasia ambazo zimekumba mashariki mwa nchi hiyo kwa takriban miaka 30. Utajiri wa madini wa DR Congo kwa sasa unatawaliwa na makampuni ya Kichina.
Bw Boulos alisema nchi yake pia ina nia ya kuchunguza madini katika nchi jirani ya Rwanda, lakini akatoa wito kwa nchi hiyo kwanza kuondoa wanajeshi wake kutoka DR Congo na kusitisha uungaji mkono wake wa kundi la M23. Rwanda inakanusha kuhusika katika mzozo huo.
Alipoulizwa iwapo Marekani ina nia ya kufaidika tu kiuchumi na Afrika na si ustawi wake, Boulos alisema “kazi yetu ni kukuza maslahi ya Marekani na kukuza ushirikiano wetu wa kimkakati”.
Trump pia amedhamiria “kumaliza vita na kuanzisha amani” kote ulimwenguni, mjumbe huyo alisema, akitaja mzozo wa Sudan kama tishio kubwa kwa serikali ya Amerika.
Bw Boulos, ambaye amehudumu kama mshauri mkuu wa Washington katika masuala ya Uarabuni na Mashariki ya Kati tangu Desemba, pia alitembelea Kenya, Rwanda na Uganda katika ziara yake.
Ana masilahi ya kibiashara barani Afrika, ikiwa ni pamoja na katika kampuni ya Nigeria ambayo inasambaza magari na vifaa Afrika Magharibi.
Mfanyabiashara huyo mzaliwa wa Lebanon alisema Trump alihisi wakati umewadia wa wa kumaliza “faida isiyo ya haki” iliyochukuliwa na washirika wengine wa kimataifa wa Afrika.
Akijibu madi katika vyombo vya habari vya Marekani kwamba utawala wa Trump una mpango kufunga balozi zake barani Afrika, Bw Boulos alisema hilo “si sahihi”, na kuongeza: “Afrika ni muhimu sana kwa Trump.”
Kuhusu ushuru wa kibiashara uliotangazwa na Trump, Bw Boulos alisema “hazina madhara yoyote” kwa nchi nyingi za Afrika kwani waligusia “kiasi kidogo cha biashara” kutoka bara hilo.
“Nchi kadhaa zimejiandaa kwa mazungumzo na mwisho wa siku tunataka haki na suluhisho la kudumu,” aliongeza.
Lesotho iliathiriwa na ushuru wa juu zaidi uliotangazwa hivi karibuni – 50% – kabla ya utekelezaji wa ushuru huokusitishwa kwa siku 90.
Imetumia Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika (Agoa) kuwa muuzaji mkuu wa nguo, ikiwa ni pamoja na jeans, kwa Marekani. Biashara hii inachangia zaidi ya 10% ya pato la taifa la Lesotho.
AGOA ilianzishwa na Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton mwaka wa 2000 ili kuhimiza biashara na uwekezaji barani Afrika lakini wachambuzi wanahofia kwamba kuna uwezekano wa kuanzishwa upya na Bunge la sasa linalotawaliwa na Republican.
Soma Pia:
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi