Tundu Lissu: Je, huu ndiyo mwisho wa Mwanasiasa huyu wa Tanzania?

Tundu

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Tundu Lissu anakabiliwa na shitaka la uhaini

  • Author, Basillioh Rukanga & Alfred Lasteck
  • Nafasi, BBC News, Nairobi & Dar es Salaam
  • Dakika 31 zilizopita

Tundu Lissu, kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, kosa ambalo adhabu yake ya juu ni hukumu ya kifo.

Alishambuliwa kwa risasi 16 katika jaribio la kumuua mwaka 2017, na tangu hapo amekuwa mmoja wa wanasiasa waliodhulumiwa zaidi nchini humo. Sasa, baadhi ya watu wanajiuliza kama huu ndio mwisho wa safari yake ya kisiasa.

Licha ya hatari kubwa inayomkabili, Lissu bado ana matumaini ya kushinikiza serikali kufanya mageuzi ya kisiasa kabla ya uchaguzi wa urais na wabunge mwezi Oktoba. Hata hivyo, hali ya kisiasa ni ngumu, na anakabiliwa na kile anachokiona kama mashtaka ya kisiasa.

Chama chake kikuu cha upinzani, Chadema, tayari kimezuiwa kushiriki katika uchaguzi huo, na yeye mwenyewe amekuwa rumande kwa zaidi ya wiki mbili.

Septemba mwaka jana, Lissu aliambia BBC kuwa hakuna kitakachokuja kwa urahisi, na kwamba ni lazima kuwa na ujasiri kudai mabadiliko “mtaani na vijijini”. Ili kutimiza malengo yake, alihisi kuwa ni lazima aongoze Chadema.

Akimlaumu mwenyekiti wa zamani Freeman Mbowe kwa kuwa mpole mno kwa serikali, Lissu alimshinda katika uchaguzi mkali wa uongozi wa chama hicho.

Baada ya miezi mitatu tu madarakani, Lissu alikamatwa na kuwekwa rumande kwa madai ya kutoa hotuba inayohamasisha wananchi kuanzisha uasi na kuvuruga uchaguzi. Hajaweza kujibu mashtaka ya uhaini lakini amekana shtaka tofauti la kusambaza taarifa za uongo.

Kabla ya kukamatwa, alikuwa akifanya mikutano mbalimbali nchini kwa kauli mbiu ya “hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi”. Anadai kuwa mfumo wa sasa umeegemea upande wa chama tawala CCM, na kwamba bila mabadiliko, hakuna maana ya kushiriki uchaguzi.

Anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Alhamisi, lakini hawezi kupata dhamana kwa sababu anakabiliwa na shtaka la uhaini.

Mawakili wake wa kimataifa wakiongozwa na Robert Amsterdam wamesema kuwa ni “jukumu lao kutetea demokrasia.” Lakini hiyo si kazi rahisi, kwani CCM imekuwa ikishinda kila uchaguzi tangu uhuru wa nchi hiyo.

Pia kuna mgawanyiko ndani ya Chadema – baadhi ya wanachama hawakubaliani na mkakati wa Lissu. Kundi la G-55 ndani ya chama hicho limechukua msimamo laini zaidi, likitaka chama kishiriki uchaguzi huku kikiendelea na mazungumzo na serikali.

ccm

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Chama cha CCM kimeshinda kila chaguzi katika historia ya Tanzania

Chama hicho kimezuiwa kushiriki uchaguzi wa Oktoba, 2025 baada ya kukataa kutii matakwa ya tume ya uchaguzi ya kusaini kanuni za maadili zinazoongoza uchaguzi huo.

Lengo kuu la kanuni hizo “ni kuhakikisha kuwa vyama vya siasa na wafuasi wao wanafuata utaratibu… na kudumisha amani na utangamano” wakati wa uchaguzi.

Chadema inaona kanuni za maadili ni njama ya kuwadhibiti wapinzani, na inahofia kuwa ukandamizaji wa serikali utaendelea.

Mwezi Septemba afisa mkuu wa chama cha Chadema alitekwa nyara na kuuawa kikatili huku kukiwa na wimbi la utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba, Chadema kililalamika kuwa maelfu ya wagombea wake walizuiwa kushiriki. CCM ilishinda takriban 98% ya viti. Serikali ilikanusha madai kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki, ikisema ulifuata taratibu zote.

Lakini kwa Lissu, uchaguzi wa serikali za mitaa ulihalalisha wito wake wa mageuzina marekebisho makubwa kabla ya uchaguzi wa urais na ubunge.

Shirika la kutetea haki za binadmu la Human Rights Watch limeelezea hofu sawa na hiyo, na limeitaka serikali kukomesha ukandamizaji wa kisiasa.

Kanisa Katoliki nalo limeongeza sauti yake kutaka Lissu aachiliwe huru bila masharti, na uchaguzi wa haki ufanyike.

Lakini kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani kumeendelea, licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuahidi mapema mwezi huu kwamba mamlaka itahakikisha usalama na haki katika uchaguzi.

BBC iliitafuta maoni ya upande wa Serikali. Mara zote imesema uchaguzi umekuwa huru na haki, na changamoto ndogondogo zinaendelea kurekebishwa, ambapo kwa sas apia imefanya marekebisho ya sheria zinazohusu uchaguzi mkuu, ikiwa pamoja na kuruhusu uwepo wa Tume huru ya Uchaguzi.

Rais Samia Suluhu Hassan amewapa Watanzania uhuru zaidi wa kisiasa baada ya kuingia madarakani kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli mwaka 2021.

Hata hivyo, Tanzania kwa mara nyingine “imeanza kuona wimbi la ukandamizajii” ambazo zilidhihirisha utawala wa Magufuli, mchambuzi wa siasa za Tanzania Nicodemus Minde anasema. Na ni katika zama hizo ambapo Lissu alinusurika katika jaribio la kuuawa.

Tanzanian police officers (in green uniform and holding guns) surround a group of young voters (all seated) following their arrest in Kigoma in 2024

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Serikali imekuwa ikituhumiwa kukandamiza upinzani

Kabla ya kukamatwa, Lissu alisema chama chake kilikuwa na orodha ya “marekebisho kadhaa muhimu ambayo lazima yafanyike ili kuhakikisha uchaguzi huru”.

Bw Amsterdam, wakili wake, aliiambia BBC kuwa hii ni pamoja na kuundwa kwa “tume ya kitaifa ya uchaguzi ambayo ni huru kweli kweli ikiwa na wajumbe wasio na uhusiano na serikali” – na hili lazima itambulike katika katiba.

Chadema pia wanadai inapotokea migogoro ya uchaguzi tume iwajibike kwa ushahidi ili kuonesha kuwa zoezi la kura lilikuwa huru na haki.

Mkakati huo wa Lissu umeingia kwenye gharama kubwa kwake na Chadema, kwani wanachama wa kundi ndani ya chama hicho linalojulikana kwa jina la G-55, limekuwa na msimamo tofati.

Kundi hilo limetoa wito kwa chama hicho kushiriki katika uchaguzi huku kikiendeleza mazungumzo na serikali kuhusu madai yake.

Hiyo ndiyo njia pia iliyochukuliwa na chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani, ACT-Wazalendo.

Pamoja na vyama 16 vya upinzani, ACT kimetia saini kanuni za maadili kuungana na chama tawala na kufanya vyama 18 vya siasa kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu nchini humo kusaini kanuni hizo. Chadema pekee ndio wamekataa.

,

Maelezo ya picha, Kulikuwa na ulinzi mkali Alhamisi ya April 24, 2025 katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi ya Lissu ilipotajwa

Lissu anaonekana kuiona nchi jirani ya Kenya, ambako maandamano makubwa mwaka jana yaliilazimisha serikali kuacha mipango ya kuongeza kodi, kama mfano wa kuigwa.

Wakati huo, aliiambia BBC kwamba Watanzania “hawajashinikiza vya kutosha kufanya mageuzi ya kidemokrasia”, na kile ambacho Kenya ilipitia ili kupata utawala [wake] wa kidemokrasia ni jambo ambalo tunahitaji kufanya”.

Iwapo mkakati kama huo utafanikiwa Tanzania haijulikani, kwani Watanzania wengi wanaonekana kusitasita kuunga mkono hadharani kampeni ambayo inaweza kuiondoa serikali.

Lakini Bw Amsterdam alisema kadiri serikali inavyokuwa haitaki mabadiliko, ndivyo itawachochea wafuasi wa Chadema “kusonga mbele na kujihusisha na uasi wa kiraia”.

Aliongeza kuwa Chadema itatumia “kila chombo cha kisheria na kisiasa” kufikia mabadiliko.

Lakini mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Thomas Kibwana alikosoa mkakati huo wa Lissu, akisema kuwa kwa muda wa bunge la sasa kumalizika Juni hakutakuwa na muda wa kutosha wa kufanya marekebisho yoyote makubwa ya kisheria kuelekea uchaguzi wa Oktoba.

Alisema huenda ni vyema Chadema wasubiri hadi baada ya uchaguzi.

Fulgence Massawe, mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za kisheria nchini Tanzania, aliiambia BBC kuwa harakati za Chadema kutaka mageuzi ya uchaguzi zinakabiliwa na vikwazo vikubwa, lakini chama hicho kina haki ya kwenda mahakamani kupinga kuenguliwa kwake katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake Mchambuzi, Nicodemus Minde alisema iwapo Chadema haitashiriki uchaguzi huo, huenda chama tawala kikaongeza wingi wa wabunge ambao tayari wapo bungeni.

Mchambuzi huyo aliongeza kuwa Chadema inaweza hata kupoteza sifa yake ya kuwa chama kikuu cha upinzani, na “bila shaka asili inarudi nyuma na pengine vyama vingine vya upinzani vitachangamkia fursa hii”.

Ni hatari ambayo Lissu na chama wamechagua kuchukua.