Chanzo cha picha, AP
Jeshi la Israeli limekiri kuhusika na mauaji ya mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kutumia mizinga, baada ya kukana kuhusika hapo awali, katika tukio lililotokea mwezi uliopita katika Ukanda wa Gaza.
Mnamo tarehe 19 mwezi Machi, mfanyakazi wa UN aliuawa baada ya eneo la Umoja wa Mataifa lililoko Deir al-Balah kuharibiwa. Wakati huo, Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilidai halikulishambulia eneo hilo.
Hata hivyo, siku ya Alhamisi, IDF ilisema kuwa matokeo ya awali ya uchunguzi wake yanaonyesha kuwa wanajeshi wake walimuua mfanyakazi huyo wa UN kwa kumtambua kimakosa kama adui, baada ya kudhani kuwa jengo hilo lilikuwa na “uwepo wa adui”.
Katika taarifa yao walisema:
“Jengo hilo lilishambuliwa kwa kuzingatia taarifa kwamba lilikuwa na wapinzani, na halikutambulika kuwa ni jengo la Umoja wa Mataifa.”
IDF iliongeza kuwa matokeo haya ya uchunguzi yameshawasilishwa kwa Umoja wa Mataifa, na uchunguzi kamili utakabidhiwa pia.
Waliongeza:
“IDF inasikitishwa sana na tukio hili zito na inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kujifunza na kutathmini hatua za ziada za kuzuia matukio kama haya siku za usoni.
“Tunatoa pole kwa msiba huu na tunawapa rambirambi familia ya marehemu.”
Tukio hilo lililosababisha kifo cha mfanyakazi wa UN raia wa Bulgaria, Marin Valev Marinov, na kujeruhi vibaya wafanyakazi wengine watano wa Umoja wa Mataifa, lilitokea siku moja baada ya Israeli kurejea katika mashambulizi dhidi ya Hamas kufuatia kusambaratika kwa usitishaji mapigano wa miezi miwili.
Pia unaweza kusoma: