Kwanini Zelensky hawezi kuiachia Urusi eneo hili?

Volodymyr Zelensky

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Author, Paul Kirby
  • Nafasi, Mhariri BBC
  • Dakika 27 zilizopita

Hapo awali Vladimir Putin alikanusha kuhusika kwa njia yoyote katika unyakuzi wa eneo la Crimea mnamo Februari 2014, wakati makomando waliovalia sare za kijani kibichi walipoliteka bunge la eneo hilo na kutawala rasi hiyo.

Hatua ya “wanajeshi hao” iliashiria mwanzo wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, ambavyo viliishia katika uvamizi kamili wa 2022.

Mustakabali wa Crimea sasa uko katikati ya mpango wa amani wa Rais Donald Trump na umemfanya Volodymyr Zelensky wa Ukraine kukataa kutambua udhibiti wa Urusi katika rasi hiyo.

Masharti kamili ya mpango wake hayajachapishwa, lakini ripoti zinaonyesha kuwa itajumuisha Marekani kutambua Crimea kama sehemu ya kisheria ya Urusi – de jure kwa Kilatini.

Kwa mujibu wa Trump, rasi ya kusini ya Ukraine “ilipotea miaka iliyopita” na “sio sehemu ya majadiliano” katika mazungumzo ya hivi punde kutafuta ya amani.

Lakini kwa Zelensky kuachana na Crimea kama sehemu isiyoweza kugawanyika ya Ukraine itakuwa ni kutojali.

Kwa maneno ya mbunge wa upinzani Iryna Gerashchenko “uadilifu wa eneo na uhuru ni mstari mwekundu kwa Ukraine na raia wake”.

Trump alitoa hoja kwamba “ikiwa [Volodymyr Zelensky] anataka Crimea, kwa nini hawakuipigania miaka 11 iliponyakuliwa na Urusi?”

Risasi chache zilifyatuliwa, lakini Crimea ilitekwa kwa mtutu wa bunduki wakati kulikuwa na umbwe wa kiutawala.

Baadaye Putin alikiri kunyakua ardhi hiyo katika mkutano wa usiku kucha na maafisa wake siku chache baada ya kiongozi wa Ukraine aliyedaiwa kuungwa mkono Urusi kuondolewa madarakani mjini Kyiv.

 Wanajeshi wasiojulikana walisemekana kuuteka mji wa Crimea lakini baadaye ilibainika wazi walikuwa Warusi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wasiojulikana walisemekana kuuteka mji wa Crimea lakini baadaye ilibainika wazi walikuwa Warusi

Crimea ni kizingiti kwa Trump

Kwa kiongozi wa Marekani ambaye yuko mbioni kufikia mkataba wa amani, Crimea huenda ikawa kizingiti.

Trump hajakosea akisema kuna uwezekano mdogo wa Ukraine kuikomboa Crimea siku za usoni, na huo ndio ukweli wa mambo – hili ni eneo ambalo limekuwa chini ya utawaliwa wa Urusi kiuhalisia. Lakini hatua hiyo bado haijatambuliwa rasmi kisheria.

Zelensky anaashiria “tamko la Crimea” la 2018 la waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Trump, Mike Pompeo.

Pompeo alisema Marekani inapinga “jaribio la Urusi kunyakua Crimea” na kuahidi kuendelea na mikakati ya kuhakikisha Ukraine inarejeshewa eneo lake.

Zelensky anachomaanisha ni kwamba Trump aliunga mkono msimamo wa Ukraine kuhusu eneo la Crimea wakati huo, na inapaswa kuzingatia hilo wakati huu.

Ikiwa unyakuzi wa ardhi ambao haujatambuliwa na jumuiya ya kimataifa utaidhinishwa na Marekani kuwa halali, hiyo itamaanisha nini kwa sheria za kimataifa na kanuni za mkataba wa Umoja wa Mataifa?

Wiki chache baada ya vita vikali vya Urusi kuanza, kulikuwa na pendekezo la awali huko Istanbul la kuweka kando suala hilo ili Urusi na Ukraine ziweze kulisuluhisha katika miaka 10-15 ijayo.

Mpango huo haukufanyika na sasa inaiona ilikuwa ni njia ya kuepuka kikwazo hicho.

Zelensky amebanwa na katiba ya Ukraine

Donald Trump (C) anaonekana kuwa na hasira, Zelensky (L) anaonekana kutokubaliana na kinachojadiliwa, huku JD Vance naye akionekana kuchoshwa na mazungumzo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump na Makamu wa Rais JD Vance wameonekana kuvurugwa na misimamo ya Zelensky

Zelensky alisisitiza kwamba hana uwezo wa kuachana na Crimea: “Hili halina mjadala. Hii ni kinyume na katiba yetu.”

Kifungu cha 2 cha katiba kinasema kwamba uhuru wa Ukraine “unajumuisha eneo lake lote” ambalo “ndani ya mpaka wake wa sasa haugawanyiki na hauwezi kukiukwa”.

Mabadiliko yoyote katika eneo la Ukraine lazima yafanyike kupitia kura ya maoni ya kitaifa, ambayo lazima iidhinishwe na bunge la Ukraine.

Sio tu Rais Trump ambaye ana shida na Kyiv. Urusi pia inaiona katiba ya Ukraine kama “kizuizi” kwa juhudi za amani.

Katiba inaweza kubadilishwa, lakini sio wakati huu ambapo Ukraine inaendeshwa chini ya sheria za kijeshi.

Putin stands with his arms outstretched in front of a Russian flag

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi Vladimir Putin