ITV, halmashauri ya Rombo katika mgogoro wa ardhi, wahusika wafunguka

Rombo. Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, imeingia katika mgogoro na Kampuni ya Independent Television (ITV) baada ya halmashauri hiyo kuinyang’anya eneo ililolimiliki tangu inaanzishwa kwake mwaka 1994.

ITV inadai eneo hilo lililopo Mkuu mjini, ndio lilikuwa na mitambo ya kurusha matangazo na uamuzi huo umesababisha Ishindwe kufunga mitambo ya kidigitali kwa ajili ya kurusha matangazo ya ITV, Radio One, Capital Redio na Televisheni.

Kampuni hiyo walipewa eneo hilo lililopo kiwanja namba 6 kitalu B Mkuu mjini mwaka 1994 wakati chombo hicho kilipoanzishwa na mwasisi wake, Reginald Mengi ilipofika mwaka 2003 walipewa barua ya toleo ya kulimiliki kwa miaka 33.

Hata hivyo, Agosti mwaka 2021, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Godwin Chacha, aliwaandikia barua ITV na Radio One, akiwajulisha kuwa barua ya toleo waliyopewa ikianzia Januari Mosi, 2003 kuwa imefutwa.

Nyaraka kuhusiana na mgogoro huo, baada ya kupewa barua hiyo ya toleo, walitakiwa kulipa kodi ya pango ya Sh64,050 kila mwaka, halmashauri iliwaelekeza kujenga majengo ya vifaa vya kudumu kwa ramani itakayopitishwa.

ITV waliweka kontena lililokuwa na vifaa vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya Sh100 milioni na kufunga mnara wa mawasiliano wa analojia lakini mgogoro huo ulipoanza ambao bado unaendelea, wameshindwa kufunga vifaa vya kidigitali.

Tangu mwaka 2021, pande hizo mbili zimekuwa zikivutana huku ITV ikidai halmashauri iliingia kwa jinai katika eneo wanalolimiliki na kuamuru waondoke bila kuwalipa fidia stahiki kama Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 inavyoelekeza.

Kulingana na ITV, kwa kuwa wao walikuwa wamiliki halali wa eneo hilo tangu 1994, hawakupaswa kuondolewa kibabe bila uwepo wa amri halali ya Mahakama na kuwa walifuata taratibu zote halali katika kumiliki eneo hilo.

Waandishi wa habari walifunga safari kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, Chacha ili kupata ufafanuzi kutoka kwa mkurugenzi huyo, lakini baada ya kiini cha safari hiyo na kutaka maelezo ya upande wa halmashauri, aliomba asilizungumzie suala hilo.

“Hilo eneo ni open space (eneo la wazi),” alisema mkurugenzi huyo na kukataa kuingia kwa undani juu ya mgogoro huo ulioanza kufukuta mwaka 2020, wakati ambao tayari ITV na Radio One wamekaa eneo hilo kwa miaka 26 mfululizo.

Walichokisema ITV

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Mkuu, yalipo makao makuu ya Wilaya ya Rombo leo Machi 3, 2025, Msimamizi wa Matangazo ya IPP Mkoa wa Kilimanjaro, Boniface Michael, alisimulia mgogoro huo ulivyoanza mwaka 2020.

“Kituo hiki cha Rombo kilianza mwaka 1994. Kwa hiyo wakati niko hapa lilitokea lile tangazo kwamba mitambo yote ya analojia izimwe kwa hiyo na sisi tulizima kwa sababu tulikuwa tunarusha matangazo ya analojia,” alisema Michael.

“Baada ya kuzima tuliendelea kukaa hivyo lakini tukawa na mpango wa kuweka redio tatu, East Africa, Radio One na Capital Radio. Wakati tuko kwenye huo mpango ndio kukaibuka mgogoro wa kiwanja na Halmashauri ya Rombo”.

Kwa hiyo, amesema walishindwa kufanya hivyo, baadaye wakaondoa mnara wa zamani na vifaa vya zamani ili waweze kuleta vifaa vingine, lakini kwa kuwa walikuwa wanasubiri mgogoro uishe ili walete lakini mgogoro huo bado unaendelea.

“Kwa hiyo, tumeshindwa kuleta vile vifaa kwa sababu kuna mgogoro na huu mgogoro wakati unaanza, yule mkurugenzi alikuja akawaondoa wale walinzi wetu waliokuwepo. Sasa tunasubiri huu mgogoro umalizike ili tulete vifaa.

“Kwa hiyo, huu mgogoro umeathiri wasilikizaji wetu wa Wilaya ya Rombo na maeneo ya jirani na tunatamani huu mgogoro umalizwe na Halmashauri ya Rombo, hata leo tufunge vifaa vya kidigitali,” amesisitiza Michael.

Michael amesema athari za mgogoro huo ni kubwa katika urushaji wa matangazo kwa kuwa walikuwa wamepanga kuleta redio ambazo zingetumia masafa yanayotumika Moshi, lakini sasa Rombo hawawezi kupata matangazo hayo.

Mmoja wa waliokuwa walinzi wa kituo hicho cha Rombo, Aniset Swai amesema anachokumbuka mwaka 2021 walifika watu wa Halmashauri ya Rombo, wakamwambia hana nafasi ya kuendelea tena na ulinzi hivyo aondoke.

“Baada ya sisi kuondoka, kulikuwa na kibanda kwa ajili ya kuwekea vifaa vya ITV, sasa baadaye wakachukua kile kibanda wakakikata ndio wakakifanya geti kwenye huo mlango wa mbele. Hawakuwa wamekuja na barua yoyote,” amesema.

“Walileta mlinzi wao mmoja akasema hapa haturuhusiwi kuendelea tena hapo watu wa ITV,” ameeleza Swai huku Aloyce Massawe aliyekuwa mfanyakazi wa ITV katika kituo hicho akilalamikia gari lake kuendelea kuhodhiwa kituoni hapo,” amesema.

 “Mwaka 2021 ulipoibuka huu mgogoro, mkurugenzi alikuja akaingilia hili eneo na kulifunga wakati huo mali za ITV zilikuwa zimehamishiwa Moshi. Mali iliyokuwa imebaki ni gari langu aina ya Kirukuu Suzuki ambalo bado linaozea humu.

“Kulikuwa pia na kibanda kilichokuwa humo ndani. Nipoachishwa kazi nilijaribu kuwaomba ITV wanisaidie nipate gari langu lakini wakasema kwa vile gari ni mali yangu binafsi basi nifuatilie mwenyewe. Hadi leo sijafanikiwa kulipata.”

Massawe ameiomba ITV isaidie kuongea na halmashauri ili arudishiwe gari lake kwani wao ni mashahidi kuwa gari ni mali yake na kwamba gari hilo ni msaada kwake kusaidia shughuli za kilimo na ufugaji kwa kuwa hana ajira tena.

Wakati halmashauri hiyo ilipolifunga eneo hilo, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye baadaye alikuja kuachishwa kazi, alikuwa ameacha gari yake ndani ya eneo hilo, na tangu Halmashauri ilifunge ameshindwa kutoa gari lake.

Ushahidi wa nyaraka

Ushahidi wa nyaraka ambazo gazeti hili linazo, unaonyesha wakati ITV na Radio One wanapewa barua ya toleo mwaka 2003, walipewa gharama zinazohitajika ili kuandaa hati ya umiliki, ambayo ni pamoja na ada ya upimaji ya Sh56,375.

ITV wakalipa gharama hizo ambazo ni Ada ya Utayarishaji wa Hati Sh8,000, ada ya ramani za hati Sh6,000, ada ya upimaji, usajili wa hati Sh12,810 na ushuru wa Serikali Sh2,50 kupitia risiti namba 12787519 na 12787520 za Novemba 4, 2003.

Desemba 1, 2020, halmashauri ikabandika tangazo katika uzio wa ITV ikisema kutokana na ukaguzi uliofanyika, imebainika baadhi ya maeneo yaliyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa vibanda, yameendelezwa kinyume na makubaliano na matumizi.

Tangazo hilo linasomeka: “Kutokana na hali hiyo, ofisi ya mkurugenzi mtendaji imeamua kusitisha mikataba yote ya maeneo yaliyowekezwa kinyume na ujenzi wa vibanda vya biashara kuanzia Desemba Mosi, 2020.”

Desemba 3, 2020, Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ikabandika tangazo katika eneo ikiwatangazia kuwa kuanzia tarehe hiyo, eneo hilo litakuwa linatumiwa na Ofisi ya Mkurugenzi baada ya mpangaji kushindwa kulipa ada ya ukodishaji wa miaka 10.

Desemba 24,2020, halmashauri ikaandaa mkataba wa upangishaji baina yake na ITV na Radio One, ambao ungeanza kutumika Januari 1,2021 hadi Desemba 31,2021, ukitaka wawe wanalipa kodi ya pango ya Sh1,500,000 kwa mwezi.

Mkataba huo ambao gazeti hili linao, unaonyesha ulishasainiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Gilbert Alex Desemba 24,2020 na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri, Godwin Chacha, aliyetia saini Desemba 28,2020.

Licha ya mkataba huo kushuhudiwa na Cornelia Bitegeko ambaye ni mwanasheria wa halmashauri, hakuna kiongozi yeyote kwa upande wa ITV na Radio One aliyesaini, kwa kile inachodaiwa hawawezi kulipa kodi ya pango mara mbili.

Hata hivyo, nyaraka zinaonesha Julai 6,2005, ITV ililipa kodi ya ardhi Sh64,050 kwa ajili ya 2005/2006 na Julai 20,2019 wakalipa Sh732,200 kama kodi ya ardhi kupitia namba ya malipo (control number) ya Serikali 991172107139.

Fedha hizo zililipwa kupitia CRDB, Tawi la Moshi na fedha hizo zilionesha zimepokewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ziliingia katika akaunti inayosomeka “Ministry of Lands Revenue,” saa 5:25 asubuhi.

Julai 15, 2021, Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ilitoa “Control number” 991174430703 kwa ITV na Radio ya Sh356,132 kwa ajili ya kodi ya ardhi, ambayo ililipwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kuanzia hapo ikawa haidaiwi.