
Katika jamii nyingi za Kiafrika kuna mila zinazotilia mkazo dhana ya uhusiano wa kifamilia na jinsi ambavyo familia zinavyoshirikiana ili kuhakikisha ustawi wa kila mmoja.
Moja ya majukumu makuu ya familia ni kuwalea watoto wao ili waweze kupata elimu bora na hata pale wanapofanikiwa, wawe chachu ya kusaidia wengine.
Hata hivyo, hali halisi ya sasa ni tofauti. Kuna idadi kubwa ya vijana wanaomaliza masomo na kupata ajira, lakini wanashindwa kurudisha fadhila kwa wazazi.
Natambua kuwa ni muhali kabisa mtoto kurudisha fadhila kwa mzazi wake, lakini kinachonishangaza ni hatua ya watoto kukosa ubinadamu wa kuwakumbuka watu waliowasaidia kufika walipo.
Hii ni changamoto kubwa katika jamii yetu ambayo nadhani suala hili sasa linahitaji mjadala wa kina na hatua madhubuti kutoka kwa Serikali.
Wito wangu kwa Serikali juu ya hili ni kutunga sheria maalumu itakayowalazimisha vijana, wanaomaliza masomo na kupata kazi, kuwahudumia na kuwajali wazazi wao kimatunzo.
Narudia kuwa hakuna mtoto anayeweza kumtunza mzazi kwa asilimia 100 kama yeye alivyolelewa, lakini inawezekana kabisa kwa mtoto kuwa na huruma ya kumtazama mzazi au mlezi wake.
Hivi inawezekanaje baba au mama anaweza kutunza watoto watano au zaidi, lakini watoto haohao washindwe kumwangalia mama au baba? Kama ubinadamu umetushinda, nadhani tujaribu msukumo wa kisheria.
Uzoefu unaonyesha vijana wengi hasa katika miji mikubwa, hawajali ndugu hasa wazazi, badala yake wamejikita zaidi kwenye familia zao walizoanzisha. Wengine wamejikita kwenye starehe na kujilimbikizia mali ambazo hata hivyo hazina msaada kwa ndugu wakiwamo wazazi.
Hili linawafanya wazazi wao, ambao kwa miaka mingi walijitahidi kutoa malezi bora na kuwapeleka shule kubaki katika lindi kubwa la umasikini.
Kitendo hicho si tu kinaibua hisia za uchungu kwa wazazi, bali pia kinakiuka dhana ya familia na mshikamano wa kijamii ya Kitanzania iliyostaarabika.
Nasisitiza Serikali kuchukua hatua ya kutunga sheria imara itakayowalazimisha vijana kuwajibika kwa wazazi wao baada ya kuajiriwa au kufanikiwa kiuchumi. Hata hivyo, sheria hii inapaswa kuzingatia mambo kadhaa muhimu:
Mosi, inapaswa kubainisha wazi majukumu ya mtoto kwa mzazi wake mara baada ya kumaliza masomo. Hii itahakikisha kwamba kila mtoto anajua haki na wajibu wake kwa wazazi wake, hasa pale anapokuwa na uwezo wa kifedha na kiuchumi.
Pili, sheria itoe ruhusa kwa wazazi kudai matunzo kutoka kwa watoto wao kama ulivyokuwa wajibu wao walipowatunza na kuwasomesha. Naamini hii itadhibiti tabia ya vijana kutowajali wazazi.
Tatu, sheria hiyo ianishe adhabu kali kwa vijana uzembe watakaoshindwa kutunza wazazi wao. Adhabu hizi zinaweza kuwa za fedha na hata kifungo kulingana na ukiukwaji wa sheria husika.
Baadhi ya nchi kama India na China tayari zimetunga sheria zinazowalazimisha watoto kuwahudumia wazazi wao pindi tu wanapopata fursa ya kujiajiri ama kuajiriwa
Aidha, sheria hizo zinatoa fursa kwa wazazi kudai matunzo kutoka kwa watoto wao na watoto ambao hawataki kutoa msaada wa kifedha, wanaweza kufunguliwa mashitaka ya kutokuwa na huruma kwa wazazi wao.
Kwa kuzingatia mifano hii ya mataifa mengine haya mawili, Tanzania inapaswa kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kwamba vijana wanawajibika kwa familia zao na wazazi wao, hali inayoweza kusaidia kupunguza watu masikini hasa vijijini.
Tunapolia ongezeko la umasikini vijijini hasa kwa wazee, tukumbuke kuwa hao ni wazazi wenye watoto wao mijini ambao kimsingi wanaweza kuwatunza kama inavyofanyika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Haiwezekani kila siku Serikali ikawa inatenga mabilioni ya fedha kusaidia watu masikini, wakati kama kutafanyika sensa, inaweza kugundulika kuwa sehemu kubwa ya wanufaika wa fedha za Tasaf wana watoto wao mijini wanaoweza kuwatunza tena hata zaidi ya kile wanachokipata kutoka serikalini.
Tuitue Serikali angalau mzigo huu wa kuwatunza masikini hasa huko vijijini. Ni ajabu mno kuona mzazi mwenye watoto watano na zaidi akitunzwa na Serikali kwa kila hali, huku pembeni kuna watoto wanaotapanya mali mijini.
Tutunge sheria hii haraka ili kudumisha maadili, mshikamano, na umoja wa familia jambo litakalosaidia kurudisha heshima kwa wazazi ambao wamejitolea kwa dhati kwa manufaa ya watoto wao.
Sanjito Msafiri ni mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi Mkoa wa Pwani. Anapatikana kwa simu 0715228898