Israeli yaua Wapalestina 34 akiwamo ofisa mwandamizi wa Hamas, mkewe

Gaza. Ofisa mwandamizi wa Hamas na mbunge wa Palestina, Salah al-Bardawil (66), mkewe na Wapalestina 32 wengine, wameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) katika mji wa Khan Younis, magharibi mwa ukanda wa Gaza.

Taarifa iliyotolewa na Hamas kupitia Al Jazeera imeripoti kuwa Salah al-Bardawil na mkewe wameuawa alfajiri ya leo Jumapili Machi 23, 2025, katika shambulio hilo la anga.

Shambulio hilo la anga ni sehemu ya mashambulizi ya kivita ya Israeli dhidi ya Gaza, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa ukali katika siku za hivi karibuni.

Wakati huohuo, Wapalestina 32 wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israeli katika maeneo mbalimbali tangu alfajiri ya Jumamosi Machi 22, 2025.

Al Jazeera imeripoti kuwa idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya Israeli katika kitongoji cha Tal al-Sultan, magharibi mwa mji wa Rafah, imeongezeka hadi watu watano.

Aidha, Wapalestina watatu, akiwemo mtoto, waliuawa na wengine kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya mizinga inayorushwa kwa vifaru vya Israeli vilivyolenga nyumba na mahema ya raia katika eneo la Al-Shimaa, Beit Lahia, Kaskazini mwa Gaza.

Miili ya waliouawa na majeruhi ilihamishiwa katika Hospitali ya Indonesia iliyopo Kaskazini mwa Gaza.

Pia, Wapalestina wawili walijeruhiwa katika shambulio la anga la Israeli lililolenga hema lililokuwa likihifadhi watu waliokosa makazi katika eneo la Mawasi, magharibi mwa Khan Yunis, Kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Mapema, shambulio la anga la Israeli lililenga nyumba katika Kitongoji cha Al-Janina, Mashariki mwa Rafah, na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.

Wizara ya Afya ya Palestina eneo la Gaza imeeleza kuwa tangu kurejeshwa kwa mashambulizi Gaza Jumanne asubuhi hadi Jumamosi, Israeli imeua Wapalestina 634 na kuwajeruhi wengine 1,172, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Huu ni mkwamo wa makubaliano ya kusitisha mapigano, ambapo Israeli imesema mashambulizi yake yanaratibiwa na Marekani.

Israeli ilikataa kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano hayo baada ya awamu ya kwanza kukamilika mapema Machi 2025.

Licha ya Hamas kutekeleza masharti yote ya makubaliano, Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu alikataa kuendelea na awamu ya pili kutokana na shinikizo kutoka kwa wapiganaji wenye msimamo mkali katika Serikali yake.

Israeli imeendelea kutekeleza mashambulizi huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023, yakisababisha vifo na majeraha ya zaidi ya Wapalestina 162,000, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, huku zaidi ya watu 14,000 wakidaiwa kutofahamika walipo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *