Israeli yatishia Hamas kwa ‘mapigano makali’ ikiwa mateka hawataachiliwa

Israeli siku ya Jumanne imetishia Hamas kwa kuanzisha tena “mapigano makali” katika Ukanda wa Gaza na kumaliza usitishaji mapigano ikiwa mateka wanaoshikiliwa katika ardhi ya Palestina hawataachiliwa ifikapo Jumamosi.

Imechapishwa:

Dakika 3

Matangazo ya kibiashara

Donald Trump, mshirika mkuu wa Israeli, aliahidi “kuliangamiza” kundi la Hamas ikiwa halitawaachilia “mateka wote” kabla ya Jumamosi “saa 6 mchana”, baada ya vitisho kutoka kwa vuguvugu hili la wanamgambo wa Kiislamu la Palestina kuahirisha zoezi la kuwaachilia huru mateka lililopangwa kwa siku hiyo kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano. Baada ya kuhamasisha wanajeshi kuzunguka Ukanda wa Gaza, ulioharibiwa na miezi 15 ya vita, siku ya Jumatatu, jeshi la Israeli limetangaza siku ya Jumanne kutuma vikosi vingine katika maeneo haya, “ikiwa ni pamoja na askari wa akiba.”

Katika hali hii ya kuongezeka mzozo, rais wa Marekani alimpokea Mfalme Abdullah II wa Jordan katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne. Mfalme huyo amesema yuko tayari kuwakaribisha watoto 2,000 wagonjwa kutoka Gaza. Usitishaji vita kati ya Israeli na Hamas, ulioanza kutumika tangu Januari 19 kwa awamu ya awali ya wiki sita, tayari umewezesha mabadilishano matano ya mateka kwa Wapalestina wanaozuiliwa na Israeli.

Lakini makubaliano haya ya usitishaji vita yamekuwa tete katika siku za hivi karibuni, wakati mazungumzo kuhusu awamu ya pili bado hayajaanza. Siku ya Jumatatu, Hamas ilitishia kuahirisha zoezi la kuachiliwa kwa mateka lililopangwa kufanyika siku ya Jumamosi, ikiishutumu Israeli kwa ukiukaji kadhaa wa makubaliano hayo. “Iwapo Hamas haitawaachilia mateka wetu ifikapo Jumamosi mchana, usitishaji vita utaisha na [jeshi la Israeli] litaanza tena mapigano makali hadi Hamas itakaposhindwa kabisa,” Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema siku ya Jumanne, bila kutaja kama alikuwa akimaanisha mateka wote au kundi dogo linalotarajiwa kuachiliwa siku ya Jumamosi.

Donald Trump, kwa upande wake, alidumisha makataa ya Jumamosi, akisema haamini kuwa Hamas wataiheshimu. Siku ya Jumatatu, alitoa wito kwa Hamas kuwaachilia “wote” mateka. “Jumamosi saa 6:00 mchana, baada ya hapo nitaliangamiza kundi la Hamas.” Hitaji hili linakwenda mbali zaidi kuliko masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo yanatoa fursa ya kuachiliwa kwa mateka 33 wakati wa awamu ya kwanza, badala ya Wapalestina 1,900. Kiongozi wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema Jumanne kwamba vitisho hivyo vitafanya “mambokuwa magumu.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa kundi la Hamas kuendelea na zoezi la kuachiliwa kwa mateka, ili “kuepusha kwa gharama yoyote kuanza tena kwa uhasama huko Gaza ambao utasababisha janga kubwa.” Makubaliano hayo hadi sasa yamesababisha kuachiliwa kwa mateka 16 wa Israeli, pamoja na Wathailandi watano nje ya makubaliano hayo, badala ya wafungwa 765 wa Kipalestina. Mnamo Februari 8, mateka watatu wa Israeli, ambao walikuwa katika hali mbaya sana ya kimwili, waliachiliwa kwa kubadilishana na Wapalestina 183. Kati ya watu 251 waliotekwa nyara katika shambulio la Hamas dhidi ya Israeil ambalo lilizusha vita mnamo Oktoba 7, 2023, 73 bado wanashikiliwa mateka huko Gaza, ikiwa ni pamoja na angalau 35 ambao walifariki, kulingana na jeshi la Israeli.

Tayari mazungumzo yanaendelea juu ya awamu ya pili ya usitishaji vita, ambayo inapaswa kuruhusu kuachiliwa kwa mateka wote, lakini serikali ya Israeli hadi sasa imekataa kuwarejesha nyuma. Hatua ya tatu na ya mwisho inapaswa kuzingatia ujenzi wa Gaza. Umoja wa Mataifa umekadiria siku ya Jumanne kwamba zaidi ya dola bilioni 53 zingehitajika kwa mradi huu mkubwa. Akimpokea Benjamin Netanyahu mjini Washington wiki iliyopita, Donald Trump alitangaza mpango wa kuiweka Gaza chini ya udhibiti wa Marekani na kuwahamisha wakazi wake nje ya eneo hilo ili kuijenga upya. Amehakikisha siku ya Jumanne kwamba hatashiriki kibinafsi katika maendeleo ya mali isiyohamishika ya Gaza. Rais wa Marekani, hata hivyo, ameonya kwamba atafikiria kusitisha misaada kwa Misri na Jordan ikiwa nchi hizi zitakataa kuwapokea Wapalestina.