
Israeli imetekeleza tishio lake dhidi ya Syria kwa kufanya mashambulizi ya anga katika maeneo yanayozunguka ikulu ya rais mjini Damascus leo Ijumaa, Mei 2, baada ya kiongozi wa jamii ya walio wachache wa Druze, wanaolindwa na mamlaka ya Israeli, kuishutumu serikali ya rais mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, kwa “mauaji ya kimbari.”
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Kiongozi wa kidini wa Druze mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Syria, Sheikh Hikmat al-Hajrin, alishutumu jioni ya Alhamisi, Mei 1, “kampeni ya mauaji ya halaiki isiyo na sababu” inayolenga “raia” katika jamii yake, kufuatia mapigano ya kidini mapema wiki hii ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 100, kulingana na shirikamoja lisilo la kiserikali.
Kisha kiongozi wa kidini wa Druze ametoa wito wa “kuingilia mara moja kwa vikosi vya kimataifa” na Israeli – jirani ya Syria ambayo iko kwenye vita na nchi hiyo na ambayo imechukua upande wa kutetea jamii ya Druze – mara moja imetishia kujibu “kwa nguvu” ikiwa Damascus haitalinda jamii hiyo ya walio wachache hawa wa kidini.
“Ujumbe wa wazi uliotumwa kwa serikali ya Syria”
Saa chache baadaye, alfajiri ya Ijumaa, “ndege za kivita zmetekeleza mashambulizi katika maeneo yanayozunguka ikulu ya rais” huko Damascus, jeshi la Israeli limetangaza kwenye Telegram. “Huu ni ujumbe wa wazi uliotumwa kwa utawala wa Syria. “Hatutaruhusu majeshi (ya Syria) kutumwa kusini mwa Damascus au kutishia jamii ya Druze kwa njia yoyote,” Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa Ulinzi, Israel Katz, wmamesema katika taarifa iliyochapishwa kwa Kiingereza na Gazeti la Times of Israel.
Hili ni zoea linalotumiwa mara kwa mara na jeshi la Israeli: shambulio la anga linalolenga eneo lililo karibu sana na eneo ambalo kwa hakika linatishiwa. Lakini jambo lisilo la kawaida kuhusu shambulio hili la Israel ni lengo halisi: ikulu ya rais huko Damascus. Hatua hii ya jeshi la anga la Israeli inakuja wakati mamia ya watu kutoka jamii ya Druze wenye asili ya Israeli waliandamana Alhamisi jioni, mwandishi wetu mjini Jerusalem, Michel Paul, anaripoti. Walizuia makutano kaskazini mwa nchi na pia walikusanyika nje ya makazi ya Benjamin Netanyahu katika mji wa Kaisaria, wakitaka atimize ahadi zake za usaidizi kwa jamii. Askari wa akiba wa Druze wametuma barua ya wazi kwa viongozi wa Israeli: “Mamia ya wapiganaji wa Druze wako tayari kujitolea mara moja kupigana pamoja na ndugu zetu nchini Syria,” wanasema.
Kuendelea kukosekana kwa utulivu nchini Syria
Mapigano karibu na kusini mwa Damascus kati ya wapiganaji wa Druze na makundi yenye silaha yanayohusishwa na utawala wa Kisunni wa Rais Ahmed al-Sharaa yanaonyesha kuendelea kukosekana kwa utulivu nchini Syria, karibu miezi mitano baada ya kupinduliwa kwa mtangulizi wake Bashar Al Assad, ambaye ani kutoka kwa jamii ya walio wachache wa Alawite. “Hatuna imani tena na chombo kinachodai kuwa serikali. (…) Serikali haiui watu wake kwa kutumia wanamgambo wake wenye msimamo mkali, na kisha, baada ya mauaji hayo, kujifanya kuwa ni watu wasiodhibitiwa,” kiongozi mmoja wa kidini kutoka jamii ya Druze ameshutumu.
Umoja wa Mataifa umehimiza “wahusika wote kujizuia zaidi” na diplomasia ya Marekani imeshutumu “vurugu za hivi karibuni na maneno ya uchochezi” dhidi ya Druze kuwa “ya kulaumiwa na yasiyokubalika.” Druze ni wachache ndani ya Uislamu wa madehebu ya Kishia. Wanachama wake wameenea kati ya Lebanon, Syria na Israeli.