
Wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina kutoka meli ya “Madleen,” iliyokamatwa na Israeli wakati ikijaribu kufika Ukanda wa Gaza, wamehamishiwa uwanja wa ndege wa Tel Aviv kwa ajili ya kurejeshwa makwao, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israeli imetangaza leo Jumanne, Juni 10, 2025.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Wale ambao wanakataa kutia saini hati za uhamisho na kuondoka Israeli watafikishwa mbele ya wizara ya mahakama kwa mujibu wa mamlaka ya Israeli,” Wizara ya Mambo ya Nje imesema kwenye mtandao wa kijamii wa X, na kuongeza kuwa wanaharakati hao wamekutana na mabalozi wa nchi zao katika uwanja wa ndege.
Meli hiyo ya Madleen ilikamatwa na Israeli siku ya Jumatatu asubuhi wakati ikijaribu kufika Ukanda wa Gaza ikiwa imesheheni msaada wa kibinadamu na wanaharakati 12 wanaounga mkono Palestina waliokuwa ndani ya meli hiyo, akiwemo mwanaharakati wa Sweden Greta Thunberg. Ilifika Jumatatu jioni katika bandari ya Israeli ya Ashdodi.
Ikisindikizwa na meli mbili za wanamaji za Israeli, meli hiyo ilifika katika bandari ya kusini mwa Israeli ya Ashdodi jioni ya siku hiyo.
Awali muungano wa Freedom Flotilla, ambao ulikodisha boti hiyo, ulithibitisha kwamba wanaharakati wake walikuwa chini ya ulinzi wa mamlaka ya Israeli na kwamba “wanaweza kuruhusiwa kuondoka Tel Aviv” mapema Jumatatu usiku.
“Tunaendelea kudai kuachiliwa mara moja kwa wafanyakazi wote wa kujitolea,” shirika hilo liliandika kwenye X, likisisitiza kwamba “kuzuiliwa kwao ni kinyume cha sheria na ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.”
Meli hiyo iliyobeba wanaharakati wa Ufaransa, Ujerumani, Brazili, Uturuki, Sweden, Uhispania na Uholanzi, iliondoka Italia mnamo Juni 1 na “kuvunja kizuizi cha Israeli” cha Gaza, ambayo iko katika hali mbaya ya kibinadamu baada ya zaidi ya miezi 20 ya vita vilivyosababishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7, 2023.