
Nchini Israeli, mvutano kati ya serikali na mahakama unaendelea. Kufuatia kufutwa kazi kwa mkuu wa idara ya upelelezi ya ndani, Baraza maalum la Mawaziri linatarajia kukutana Jumapili, Machi 23, kuanzisha mchakato wa kumfukuza kazi Mshauri wa sheria Mkuu wa serikali, ambaye pia ni mwanasheria mkuu. Kwa kufanya hivyo, wengi wanamtuhumu Benjamin Netanyahu kwa mgongano wa kimaslahi, kwani waziri mkuuanakabiliwa na uchunguzi kuhusu ufisadi.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Jerusalem, Michel Paul
Hii ni barua kali kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Israeli kwa mawaziri: Gali Baharav-Miara anaishutumu serikali kwa kutaka kujiweka juu ya sheria na kufanya kazi bila kuchunguzwa na kuwepo na usawa. Anaelezea mkutano huu wa serikali kwa kufukuzwa kwake mwenyewe kama batili kisheria. Madhumuni halisi ya utaratibu huo, anaongeza, ni kufumbia macho vitendo visivyo halali vinavyofanywa na serikali.
Mawaziri wa Israeli wamepiga kura kwa kauli moja kuanza mchakato wa kumuondoa madarakani mwanasheria mkuu huyo. Waziri wa Sheria Yariv Levin, ambaye ameongoza kikao hicho, amesikitika sana kwamba Gali Baharav-Miara hakuhudhuria mkutano huo au kutuma mwakilishi. “Huu ni ushahidi zaidi wa dharau kubwa anayoionyesha kwa serikali na wajumbe wake,” amesema.
Baraza la mawaziri la Israeli limekutana bila kiongozi wa serikali. Benjamin Netanyahu ana mgongano wa kimaslahi katika kesi hizi kutokana na kesi yake ya ulaghai, uvunjaji wa uaminifu na ufisadi.
Mchakato wa kumuondoa madarakani unaotafutwa na serikali unapaswa kuchukua angalau miezi miwili, kulingana na wataalam wa sheria. Utafanyika kwa hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa tume maalum, wakati ambapo katiba ya nchi tayari ina matatizo.
Na mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu mjini Jerusalem, maelfu ya waandamanaji wameandamana kwa kelele kupinga kile wanachosema ni kuvunjika kwa mfumo wa kidemokrasia.