Ndege za kivita za Israel zimeshambulia kwa mabomu jengo la makazi ya raia linalowahifadhi Wapalestina waliolazimika kuhama makazi yao kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.
Ripoti zinasema raia wa Kipalestina wasiopungua 77 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameuliwa katika mashambulizi ya kinyama ya ndege za kivita za Israel dhidi ya jengo la ghorofa tano katika mji wa Bait Lahia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza leo Jumanne.
Ripoti zinasema kuwa makumi ya watu wamefunikwa na vifusi vya jengo hilo lililoporomoshwa katika mashambulizi ya ndege za kivita za Israel leo Jumanne. Hadi tunaingia mitamboni, watoa huduma za uokoaji walikuwa wakiendelea kufukua vifusi kutafuta manusura.

Wakati huo huo, Dr. Hussain Abu Safia Mkurugenzi wa Hospitali ya Kamal Adwan ameiambia televisheni ya al Jazeera kuwa makumi ya raia wa Kipalestina waliojeruhiwa katika hujuma ya kikatili ya ndege za kivita za Israel huko Bait Lahia wamefikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu na kwamba wengi wanaweza kupoteza maisha kutokana na uhaba wa vifaatiba na dawa.
“Jamii ya kimataifa inapasa kuchukua hatua za kuwasaidia Wapalestina na si kutazama tu mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa kizayuni huko Gaza,” amesisitiza Dr. Hussain Abu Safia Mkurugenzi wa Hospitali ya Kamal Adwan huko Gaza.