Israel yafanya mauaji mengine ya halaiki Ghaza, yawaua shahidi Wapalestina wasiopungua 96

Wapalestina wasiopungua 96 wameuawa shahidi na wengine 60 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya anga yaliyofanywa leo na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kaskazini na katikati mwa Ukanda wa Ghaza.

Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina huko Ghaza imetangaza kuwa ndege za kivita za Israel zimelenga majengo kadhaa ya makazi na nyumba katika mji wa kaskazini wa Beit Lahia na kambi za wakimbizi za Nuseirat na Bureij katikati mwa ukanda huo.

Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo imesema, zaidi ya watu 72 wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo ya Beit Lahia, na Wapalestina wengine 24 wameuliwa shahidi na wengine 60 wamejeruhiwa katikati mwa Ghaza.

Taarifa ya ofisi hiyo ya habari imefafanua kuwa, jeshi vamizi la kizayuni limefanya mauaji hayo ya halaiki huku likiwa linajuwa kwamba makumi ya raia waliolazimika kuhama makazi yao walikuwa ndani ya majengo hayo, na kwamba wengi wao walikuwa watoto na wanawake ambao walikuwa wamelazimika kuhama makazi yao katika vitongoji vyao.

Jinai za Israel Ghaza hazina mfano

Kadhalika, Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imeitaka jamii ya kimataifa kukemea, mauaji hayo ya kutisha dhidi ya raia waliolazimika kuhama makazi yao na kuuwajibisha utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa.

Kabla ya taarifa hiyo, duru moja ya kitiba ilivieleza vyombo vya habari kuwa makombora ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni yamepiga jengo la ghorofa tano katika eneo la Beit Lahia mapema leo na kuua shahidi watu wanaokaribia 50 na kuwaacha wengine kadhaa wamenasa chini ya vifusi.

Mashuhuda wamesema, zaidi ya raia 70 waliolazimika kuhama makazi yao walikuwa wamepewa hifadhi ndani ya jengo hilo.

Wapalestina wapatao 43,800 wameuawa shahidi huko Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine zaidi ya 103,600 wamejeruhiwa tangu jeshi la utawala wa Kizayuni lilipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo hilo mnamo Oktoba 7, 2023 …/