Israel yadai kumuua kiongozi mwandamizi wa Hamas, jeshi laizingira Gaza

Gaza. Jeshi la Israel (IDF) limedai kuwa kiongozi Mwandamizi wa Hamas ameuawa katika operesheni ya pamoja na Shirika la Kijasusi la Israel (Shin Bet).

Kupitia chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii, IDF imeeleza kuwa msaidizi huyo wa Kamanda wa Brigedi ya Gaza ya Hamas aliuawa siku kadhaa zilizopita katika shambulio mjini Gaza nchini Palestina.

Al Jazeera imeripoti leo Jumatano Aprili 16,2025, kuwa Jeshi hilo limesema kuwa mtu huyo aliyefahamika kama Mahmoud Abu Hasira alihusika katika operesheni ya Julai 2014 ambapo wapiganaji wa Hamas walivamia jengo lililokuwa limeimarishwa baada ya kuingia kupitia kwenye handaki, na kuwaua wanajeshi watano wa Israel huku wakimjeruhi mwingine mmoja.

Vyombo vya habari vya Kipalestina vimeripoti kuwa helikopta za kivita za Israel zinashambulia mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza, na mji wa Abasan al-Kabira pia umeshambuliwa kwa mizinga mizito na jeshi la Israel katika eneo la karibu la Khan Younis ukanda huo.

Mashambulizi ya mizinga pia yameripotiwa katika kipindi cha saa 24  zilizopita katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza, pamoja na kambi ya Bureij.

Taarifa za awali zilionyesha watu watatu waliuawa katika shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza mapema asubuhi hii, na wengine sita kuuawa usiku katika shambulio la Israel dhidi ya familia ya Hassouna katika mtaa wa Tuffah, mjini Gaza.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Israel limethibitisha kuwa lilitekeleza shambulio kusini mwa Lebanon usiku wa Jumanne, likidai lilikuwa likilenga Hezbollah.

Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Jeshi la Israel limeishutumu Hezbollah kwa kutumia miundombinu ya kiraia kwa njia ya kijanja na kuwafanya wakazi wa Lebanon kuwa kinga ya binadamu.

Shambulio hilo la hivi karibuni limekuja baada ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa vikosi vya Israel vimewaua takriban raia 71 nchini Lebanon, tangu kuanza kwa kusitishwa kwa mapigano na Hezbollah mnamo Novemba.

Pia hali ya hofu imeibuka baada ya tawi la kijeshi la Hamas kusema kuwa limepoteza mawasiliano na kundi lililokuwa likimlinda mwanajeshi wa Marekani na Israel, Edan Alexander, baada ya Israel kulenga eneo alikokuwa akishikiliwa kwa mashambulizi ya moja kwa moja.

Kwa mujibu wa vyanzo vya matibabu vya Gaza takriban watu 23 wameuawa katika mashambulizi ya Israel kote Ukanda wa Gaza tangu alfajiri ya Jumanne, na taarifa kuhusu mashambulizi na vifo zaidi zinaendelea kutolewa.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mapema jana alifanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Ukanda wa Gaza kuangalia maendeleo ya operesheni za kijeshi za IDF.

Netanyahu alitumia ziara hiyo kuelezea msimamo wa Iran chini ya kiongozi wake Ayatollah Ali Khamenei kuwa utaliponza taifa hilo badala yake linapaswa kuachana na mpango wake wa urutubishani wa nyuklia na kusema kuwa isipofanya hivyo, Israel haitosita kuanzisha mashambulizi katika taifa hilo.

Wizara ya Afya ya Gaza chini ya Hamas imeeleza takriban Wapalestina 51,000 wamethibitishwa kuuawa na 116,343 kujeruhiwa katika vita vya Israel dhidi ya Gaza tangu kuanza kwake miezi 18 iliyopita.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *