Utawala wa Kizayuni wa Israel umekiri kuuawa askari wake 890 tangu kuutekelezwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa na kisha kuuanza vita dhhidi ya Gaza.
Wizara ya Vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza katika taarifa yake kwamba, tangu tarehe 7 Oktoba 2023, maafisa na askari 890 wa jeshi, polisi na vyombo vya usalama vya utawala huu wameuawa.
Baadhi ya duru zinasema kuwa, idadi ya askari wa Israel walioangamizwa hadi sasa ni kubwa kuliko hii iliyotangazwa.
Wakati huo huo, ripoti zinaeleza kuwa, jeshi la utawala ghasibu wa Israel limepata hasara kubwa katika vita vya ardhini huko Lebanon baada ya wanajeshi wake 70 kuuawa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, wanajeshi wengine wengi wa Israel wamejeruhiwa huku baadhi yao wakiwa mahututi, wakati wa makabiliano hayo yaliyofuatia mashambulizi ya kuvizia ya Hizbullah, na kuongeza kwamba kuna udhibiti mkali uliowekwa na jeshi la Israel karibu na eneo yalipojiri mapigano hayo.
Ikumbukwe kuwa, tangu tarehe 7 Oktoba 2023 na kwa uungaji mkono kamili wa nchi za Magharibi, utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mauaji makubwa na ya kinyama katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina, na kimya cha jamii ya kimataifa na taasisi za kutetea haki za binadamu mbele ya jinai za Israel zimepelekea kuendelezwa mauaji hayo yanayowalenga zaidi wanawake na watoto wa Kipalestina.