
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amemchagua aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Wanamaji Eli Sharvit kuwa mkuu mpya wa Shin Bet, ofisi yake imesema siku ya Jumatatu, licha ya Mahakama ya Juu kuzuia ombi la serikali la kumwondoa mkurugenzi wa sasa wa idara ya usalama wa ndani.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Baada ya kufanya mahojiano ya kina na wagombea saba waliohitimu, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameamua kumteua Kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji, Admiral Eli Sharvit, kuwa mkurugenzi wa Shin Bet,” Ofisi ya Waziri Mkuu imesema katika taarifa yake.
“Admiral Sharvit alihudumu kwa miaka 36 katika Vikosi vya Ulinzi vya Israeli, ikiwa ni pamoja na miaka mitano kama Kamanda wa Jeshi la Wanamaji. Katika nafasi hii, aliongoza maendeleo ya kikosi cha ulinzi wa baharini (…) na kusimamia mifumo tata ya uendeshaji dhidi ya (vuguvugu la Kiislamu la Palestina) Hamas, (vuguvugu la Kiislamu la Lebanon) Hezbollah na Iran,” imeongeza taarifa hiyo.
Uteuzi wa kushangaza
Huu ni uteuzi wa kushangaza, kulingana na wachambuzi wengi nchini Israeli. Kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Israeli Eli Sharvit ni afisa wa ngazi ya juu wa akiba ambaye hajahudumu kwa zaidi ya miaka saba na hana ujuzi maalum wa ujasusi wa ndani, anaripoti mwandishi wetu huko Jerusalem, Michel Paul. Benjamin Netanyahu, kulingana na taarifa kutoka ofisi yake, alifanya mahojiano ya kina na wagombea saba kabla ya kufanya uamuzi huu.
Waziri Mkuu wa Israeli aliamua kumfukuza kazi mkuu wa Shin Bet, Ronen Bar, akitaja “kupoteza uaminifu wa kitaaluma na kibinafsi kati ya Waziri Mkuu na mkurugenzi wa idara hiyo” ambayo inazuia “serikali na Waziri Mkuu kutekeleza mamlaka yao kikamilifu.”
Mahakama ya Juu ilisitisha kuachishwa kazi kwa Ronen Bar Lakini kufuatia maombi yaliyowasilishwa na upinzani wa Israeli na shirika moja lisilo la kiserikali, Mahakama Kuu mnamo Machi 21 ilisitisha uamuzi wa serikali wa kumfuta kazi Ronen Bar, ikisubiri mapitio ya rufaa ifikapo Aprili 8. Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo, Gali Baharav-Miara, ambaye pia anahudumu kamamshauri wa masuala ya kisheria wa serikali, alimuonya Benjamin Netanyahu kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu “unamkataza” kwa muda kumteua mkuu mpya wa Shin Bet.
Lakini Benjamin Netanyahu alisisitiza kuwa ni juu ya serikali yake kuamua ni nani ataongoza idara ya usalama wa ndani.
Uamuzi wa kumfukuza kazi mkuu wa Shin Bet ulizua maandamano makubwa nchini Israeli. Baadhi ya Waisraeli wanashutumu kile wanachokiona kuwa ni mwelekeo wa kiimla wa Waziri Mkuu, ambaye anaongoza mojawapo ya serikali za mrengo wa kulia katika historia ya Israeli.