Jeshi la Israel (IDF) limethibitisha kuwa limeupata mwili wa Mohammed Sinwar, kiongozi wa ngazi ya juu wa Hamas, ambaye anasadikiwa kuwa mkuu wa wanamgambo wa kundi hilo ndani ya Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP, IDF ilisema: “Katika operesheni maalum… na baada ya kukamilika kwa mchakato wa utambuzi, sasa imethibitishwa kuwa mwili wa Mohammed Sinwar umepatikana ndani ya njia ya handaki chini ya Hospitali ya Ulaya mjini Khan Yunis.”
Msemaji wa jeshi, Effie Defrin, alisema uchunguzi wa vinasaba (DNA) na ukaguzi mwingine umebaini kuwa mwili huo ni wa Sinwar. Gazeti la Times of Israel limeripoti kuwa miili mingine iliyopatikana bado inafanyiwa utambuzi.
Israel ilitangaza awali kwamba Sinwar “ameuawa” mnamo Mei 13, ingawa Hamas haijathibitisha wala kukanusha taarifa hizo.
Israel yaapa kuizuia meli ya misaada ya Greta Thunberg kuingia Gaza
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema jeshi limeagizwa kuizuia meli ya misaada ya kibinadamu, Madleen, inayoelekea Gaza ikiwa na mwanaharakati wa mazingira kutoka Sweden, Greta Thunberg, pamoja na wanaharakati wengine 11.
Meli hiyo, inayotumia bendera ya Uingereza, ni sehemu ya muungano wa Freedom Flotilla Coalition (FFC) na iliondoka Sicily wiki iliyopita ikiwa na vifaa muhimu vya misaada kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao umekuwa chini ya mzingiro wa Israel.
“Nimeagiza IDF kuhakikisha kuwa meli ya Madleen… haifikii Gaza,” alisema Katz. “Kwa Greta na marafiki zake wanaotetea propaganda za Hamas, nasema wazi: ni bora mrudi nyuma, hamtaingia Gaza.”
Rima Hassan, mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Ufaransa na mmoja wa waliomo ndani ya meli hiyo, alisema: “Tutasalia tukiwa tumehamasika hadi dakika ya mwisho — hadi pale Israel itakapozima mitandao ya mawasiliano.” Aliongeza kuwa: “Kuna raia 12 ndani ya meli. Hatuna silaha. Tuna msaada wa kibinadamu pekee.”
Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa jeshi linapanga kuikamata meli hiyo kabla haijafika Gaza na kuielekeza kwenye bandari ya Ashdod, kisha kuwarejesha nyumbani wahusika.
Iran yadai kupata nyaraka za siri za mpango wa nyuklia wa Israel
Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa mashushushu wa taifa hilo wamefanikiwa kupata nyaraka nyeti mno kuhusu mpango wa nyuklia wa Israel na mikakati yake ya kitaifa ya ulinzi.
“Ingawa operesheni ya kupata nyaraka hizi ilitekelezwa miezi kadhaa iliyopita, idadi kubwa ya nyaraka na changamoto za kuzisafirisha kwa usalama hadi maeneo ya ulinzi ndani ya Iran zilisababisha uamuzi wa kuweka siri taarifa hii hadi sasa,” iliripoti PressTV, ikinukuu vyanzo vya serikali visivyotajwa majina.
Taarifa hiyo ilidai kuwa kiasi cha nyaraka, picha na video ni kikubwa kiasi kwamba uchambuzi wake umechukua muda mrefu. Serikali ya Israel haijatoa kauli rasmi kuhusu dai hilo.
Iran na Israel zimekuwa zikihusika katika vita vya kijasusi kwa miongo kadhaa, huku Iran ikikataa kuitambua Israel kama taifa, na Israel ikilenga kuizuia Tehran kupata silaha za nyuklia.
Vita hivi vya kijasusi vinahusisha mashambulizi ya kimtandao, matumizi ya droni, hujuma za moja kwa moja, na mauaji ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran.
Chanzo: AFP, DPA, RTRE,APE