Israel kuendelea kuishambulia Hezbollah

Israel kuendelea kuishambulia Hezbollah

Hii ni baada ya kushambulia kusini mwa Beirut katika kile ambacho viongozi wa Lebanon wanakiita ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya usitishaji mapigano ya mwezi Novemba.

Israel jana ilitoa mwito kwa wakaazi wa kusini mwa Beirut kuondoka katika eneo hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran na muda mfupi baadaye, makundi ya watu yakalikimbia eneo hilo wakihofia maisha yao.

Takribani saa moja baadaye, kulirindima mashambulizi yaliyopelekeamoshi mkubwa kufuka katika anga ya mji wa Beirut. Mashambulizi haya yamefanyika miezi sita baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah.

Vituo vya misaada kutokaribiwa

Katika taarifa, waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema hakutokuwa na utulivu au amani Beirut bila usalama kwa taifa la Israel.

Kwengineko kundi moja litoalo misaada Gaza linaloungwa mkono na Marekani na Israel limesema leo kuwa vituo vyake vyote vya usambazaji misaada vimefungwa kwa muda usiojulikana.

Gazastreifen | Hilfslieferung der Gaza Humanitarian Foundation GHF
Malori ya misaada ya kiutu yakiingia Gaza Picha: Gaza Humanitarian Foundation/REUTERS

Kundi hilo la Wakfu wa Kiutu wa Gaza, GHF, limewataka raia wa Gaza kutokaribia chochote kati ya vituo vya misaada kwa ajili ya usalama wao, kufuatia msururu wa mashambulizi ya risasi katika siku chache zilizopita.

Kundi hilo ambalo wiki iliyopita lilianza kutoa misaada ya chakula kwa Wapalestina walio na njaa ndani ya Ukanda wa Gaza, limesema tarehe ya kufunguliwa kwa vituo hivyo itatangazwa baadae.

Hayo yakiarifiwa Wapalestina wamekuwa na wakati mgumu kuadhimisha mojawapo ya sikukuu muhimu zaidi katika Uislamu, Eid al-Adha.

Hii ni kutokana na hatua ya Israel kuzuia kuingia katika Ukanda wa Gaza kwa shehena za nyama na vyakula vingine kwa kipindi cha miezi mitatu sasa. Israel imechukua hatua hiyo kwa ajili ya kuwashinikiza wanamgambo wa Hamas, kuwaachia mateka walio mikononi mwao kufuatia lile shambulizi la Oktoba 7.

Kwa kawaida Waislamu huchinja kondoo au ng’ombe katika sikukuu hii na kuwapa maskini sehemu ya kile walichokichinja kama sadaka.

Umoja wa Ulaya washikamana na mahakama ya ICC

Katika taarifa inayofungamana na mzozo huo, Marekani imewawekea vikwazo majaji 4 wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutokana na waranti wa kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu walioutoa.

Majaji hao 4 ambao wote ni wanawake, sasa hawatokubaliw akuingia Marekani na mali zozote wanazomiliki katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, zitafungiwa. Hatua hizo aghalabu huchukuliwa dhidi ya waunda sera na wala si dhidi ya maafisa wa mahakama.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mara baada ya tangazo hilo la vikwazo kutolewa, Umoja wa Ulaya kupitia kwa mkuu wa Baraza la Ulaya Antonio Costa, umesema kwamba unaiunga mkono mahakama ya ICC, ukisema ni kiungo muhimu kwa haki ya kimataifa.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake mjini New York, Human Rights Watch, limetoa wito kwa mataifa mengine kupaza sauti na kuonyesha kujitegemea kwa mahakama ya ICC ambayo iliundwa mwaka 2002 ili kuwafungulia mashtaka watu wanaohusika na uhalifu mbaya zaidi duniani, endapo nchi zenyewe haziwezi kufanya hivyo.

Vyanzo: AFP/Reuters

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *