Vyombo vya habari vya Kiebrania vimetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unataka kufikia makubaliano na harakati ya Hamas yatakayowezesha kuachiliwa idadi ndogo ya mateka wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Ghaza mkabala na kusitishwa mapigano kwa muda wa mwezi mmoja.
Gazeti la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa, katika mikutano iliyofanyika Jumapili na Jumatatu katika mji mkuu wa Qatar, Doha, mkuu wa shirika la ujasusi la Israel Mossad, David Barnea alishauriana na mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani (CIA) William Burns na Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani kuhusu kufanikisha kufikiwa makubaliano kati ya Israel na harakati ya Muqawama wa Palestina ya Hamas juu ya pendekezo hilo.
Gazeti hilo limesema, Barnea alipendekeza kuachiliwa mateka 11 hadi 14 wa Israel, wakiwemo wanawake na wazee waliosalia, ili mkabala wake vita vinavyoendelezwa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Ghaza visitishwe kwa muda wa siku 30.

Kwa mujibu wa pendekezo hilo, Israel itawaachilia wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela zake, lakini idadi halisi ya watakaoachiwa itawekwa mezani kwa majadiliano.
Ripoti hiyo ya gazeti la Yedioth Ahronoth imeongeza kuwa pendekezo hilo litawasilishwa hivi karibuni kwa viongozi wa Hamas ili kutathmini kama harakati hiyo ya Muqawama itakuwa tayari kurejea kwenye mazungumzo kwa ajili ya “mpango mdogo” wa makubaliano.
Baadhi ya duru za Kizayuni zimelieza gazeti hilo kuwa ili kuifanya Hamas ilikubali pendekezo lisilojumuisha kipengee cha kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Ghaza, itabidi utawala huo wa Kizayuni ukubali kuwaachilia wafungwa wengi zaidi wa Kipalestina kuliko vile ambavyo ungepaswa…/