
Idara ya Yyombo vya Habari katika Ukanda wa Gaza, ambako utawala wa Israel umekuwa ukiendesha vita vya mauaji ya kimbari tangu Oktoba mwaka jana, inasema waandishi wa habari 188 wa Kipalestina wameuawa shahidi tangu kuanza kwa mashambulizi hayo ya kikatili ya kijeshi.
Idara hiyo ilitoa takwimu hiyo siku ya Jumamosi, ikiwataja wanahabari wanne kama waathiriwa wa hivi majuzi zaidi wa mashambulizi hayo.
Imewatambulisha wanne kuwa ni Zahraa Mohammad Abu Sukheil, Ahmad Mohammad Abu Sukheil, Mustafa Khadr Bahar, na Abdel Rahman Khadr Bahar.
Idara hiyo imesema “inalaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel kuwalenga na kuwaua waandishi wa habari wa Kipalestina na kwamba utawala huo unabeba dhima ya uhalifu huo wa kutisha.”
Aidha idara hiyo imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, mashirika ya kimataifa, na wale wanaojihusisha na kazi ya uandishi wa habari duniani kote kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Israel na kuushinikiza ili ukomeshe mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina sambamba na kuufikisha utawala huo katika mahakama za kimataifa.
Idara ya Vyombo vya Habari katika Ukanda wa Gaza pia imesema utawala na Marekani, kama mshirika mkubwa wa Israel, pamoja na nchi nyingine zinazosaidia mauaji ya kimbari zinahusika kikamilifu katika jinao za utawala huo ghasibu.
Takriban Wapalestina 43,552, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa na wengine 102,765 kujeruhiwa tangu Israel ianzishe vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza Oktoba 7 mwaka jana.