Israel imefanya kosa kubwa la kiistratijia kuua kigaidi makamanda wa Muqawama

Balozi wa Iran nchini Lebanon amesema kuwa, jinai ya utawala wa Kizayuni ya kuwaua kigaidi makamanda wa Muqawama ni kosa kubwa la kiistratijia na kusisisitiza kuwa, Israel haiwezi kuimaliza nguvu Hizbullah kwa kuwaua kigaidi makamanda wake.

Balozi Mojtaba Amani amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na Kanali ya Kwanza ya televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, hivi sasa wanamapambano wa Hizbullah wanapambana kwa ari kubwa zaidi na wanatoa vipigo vikali zaidi kwa utawala wa Kizayuni, hivyo Israel imefanya kosa kubwa la kimkakati kuwaua kigaidi makamanda wa Muqawama.

Balozi wa Iran nchini Lebanon vile vile amesema kuwa, hivi sasa hakuna nafasi yoyote ya juu ya Hizbullah iliyobaki wazi bila ya kujazwa na kiongozi mwengine na kwamba vipigo vinavyotolewa na harakati hiyo ya Muqawama katika medani za mapambano dhidi ya Wazayuni ni ushahidi wa uhakika huo.

Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliyeuliwa kigaidi na Israel

Balozi Amani amehoji akisema: Hivi Wazayuni hawaoni ni kwa kasi kubwa kiasi gani Hizbullah imeweza kujijenga upya tena haraka mno baada ya kuuliwa kigaidi makamanda wake wa ngazi za juu?

Aidha amesema: Hizbullah ina historia ya miaka 45 ya kupambana na utawala wa Kizayuni na katika muda wote huo imeweza kujioanisha vizuri na mazingira ya kila namna hata mazingira magumu kupindukia. Muda wote inakuwa na nguvu zaidi kadiri inavyokabiliwa na misukosuko na hiyo ndiyo dhati ya kambi ya Mugawama.

Vilevile amesema kuwa, sababu kuu inayopelekea utawala wa Kizayuni ukwame kwenye kinamasi ni kutokuwa na washauri wenye uzoefu tofauti na ilivyo kambi imara ya Muqawama.