
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Mashujaa FC, Ismail Mgunda ameanza rasmi mazoezi ya kuitumikia AS Vita ya DR Congo iliyomsajili hivi karibuni baada ya kukamilisha taratibu zote zilizotakiwa nchini humo.
Mgunda ametua AS Vita inayonolewa na kocha wa zamani wa Azam FC, Youssouf Dabo ni miongoni mwa wachezaji watano wapya waliosajiliwa na timu hiyo akiwamo nyota wa zamani wa Yanga, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema tayari amekamilisha taratibu za usajili na ameanza mazoezi na wachezaji wenzake licha ya timu hiyo bado haijamtambulisha.
“Bado sijatambulishwa lakini kweli tayari nimeshajiunga na nimeshaanza mazoezi, nimefurahi kufanikisha dili hilo,” alisema Mgunda ambaye alifunga mabao mawili ya Ligi Kuu msimu huu.
Kuhusu ukaribu wake na Skudu alisema; “Nimemfahamu kabla hata hajaja Yanga, tulikutana Afrika Kusini wakati nafanya mazoezi na Highlands Parks, yeye alikuwa anacheza hapo nilikaa nao kama miezi sita na sasa tumekutana tena ni mtu aliyenipokea na tunashauriana vitu vingi.”
Mbali na Skudu na Mgunda, As Vita iliyong’olewa raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na Stellenbosch ya Afrika Kusini, pia imewasajili Yannick Bangala aliyewahi kutamba na Yanga na Azam FC kabla ya kutemwa dirisha dogo la msimu huu kumpisha Allasane Diao aliyekuwa nje ya uwanja kwa sababu ya majeraha.
Wendine ni Denis Modzaka aliyekuwa akiitumikia Coastal Union na kipa kutoka Uganda, Said Keni aliyekuwa akiidakia Shashamane City ya Ethiopia.