
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, ushirikiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unaendelea katika fremu ya mkataba wa Kuzuia Utengenezaji na Usambazaji wa Silaha za nyuklia NPT na haki za kimataifa.
Muhammad Islami amesema hayo leo katika mkutano wakke na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ambapo ameyatathmini mazungumzo yake na Grossi kwamba, yalikuwa chanya.
Islami amesisitiza: Mkutano wa leo ni muhimu sana wakati huu, hasa kwa vile heshima ya mashirika ya kimataifa inaharibiwa na propaganda za kisaikolojia za mfumo wa kibeberu, na tunamtaka Mkurugenzi Mkuu asiruhusu harakati hii ya kufurutu ada ipenyye na kuwa na ushawishi wa kutoa azimio la kuingilia mambo na hivyo kuathiri uhusiano kati ya Iran na IAEA.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki akijibu swali kuhusu toshio la utawala wa Kizayuni la kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran, amesema: Nilisema wazi kwamba mitambo hiyo haipaswi kushambuliwa kwa sababu ina matishio ya kimazingira na kibiolojia.