Ishu ya Sancho na Man United, Chelsea hii hapa

Staa wa Manchester United, Jadon Sancho ameambiwa anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha kocha Ruben Amorim endapo kama atafiti kwenye mfumo wa kocha huyo.

Staa huyo wa England ametumikia msimu huu kwa mkopo huko Chelsea, lakini hatujui hatima ya maisha yake baadaye baada ya miamba hiyo ya Stamford Bridge kugomea ishu ya kumchukua jumla.

Chelsea inakabiliwa na makubaliano ya kumchukua Sancho jumla kwa ada ya Pauni 25 milioni endapo kama timu hiyo itamaliza nafasi ya 14 au ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu.

Hata hivyo, kwenye makubaliano hayo, Man United imeweka kipengele kinachowahitaji kulipa kiasi kidogo sana cha pesa ili kusitisha mpango wa Sancho kujiunga jumla Stamford Bridge.

Huko kwenye kikosi cha Chelsea, Sancho ameasisti mara tatu katika mechi zake tatu za kwanza kwenye ligi na kisha alifunga kwenye ushindi wa mara mbili mfululizo Desemba mwaka jana, lakini baada ya hapo ameshindwa kufanya kitu cha maana uwanjani.

Baada ya kumshuhudia Sancho akicheza zaidi ya miezi miwili bila ya kufunga wala kuasisti, staa wa zamani wa Chelsea, William Gallas alisema mchezaji huyo anapaswa kuondoka na kwenda kucheza kwingineko msimu ujao.

“Sijui tatizo ni nini, lakini kwa sasa hapaswi kubaki Chelsea kwa sababu anahitaji kufanya zaidi,” alisema beki huyo wa zamani wa Ufaransa.

Kurudi kwenye klabu yake ya Man United isingewezekana kipindi cha Erik ten Hag, lakini sasa Kocha Amorim anaweza kumfungulia milango. Na kocha wa zamani wa Sancho, anaamini mchezaji huyo ana nafasi ya kupata namba akirudi Old Trafford.

“Jadon anaweza kucheza kama Namba 10 wa upande wa kushoto, sijawahi kumwona akicheza wing-back,” alisema Dan Micciche, kocha aliyemnoa Sancho kwenye timu ya vijana ya England na kuongeza. “Je, anaweza kucheza nafasi hiyo? Ndiyo, bila shaka. Nadhani anaweza kucheza kwenye mfumo wa Ruben Amorim.”

Chelsea bado haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya Sancho juu ya maisha yake huko Stamford Bridge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *