Ishu ya ‘hatuchezi’ ya Yanga yatinga CAS, kesi ya msingi ipo

Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo CAS imeanza kufanya mambo yake ikiwasiliana rasmi na wahusika wakuu kesi ya klabu ya Yanga iliyofungua shtaka ikipinga pamoja na mambo mengine kuahirishwa kwa dabi ya Kariakoo Machi 8.

Kikanuni mawasiliano hayo yanamaanisha kuna kesi ya msingi baada ya kuiridhidha CAS na ndio sababu ya kuwasiliana na watajwa kwani maranyingi kesi ikiwa haina mashiko huwasiliana na mhusika pekee kumueleza.

CAS imewasiliana rasmi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikianza kulifanyia kazi shauri lililofunguliwa na Yanga ikipinga maamuzi ya kuahirishwa kwa mchezo wa Ligi namba 184 dhidi ya Simba.

Kwenye barua ambayo Mwanaspoti imejiridhisha ni kwamba CAS imezitaka Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), TFF na Simba kuwasilisha vielelezo vyao juu ya shauri hilo ndani ya siku kumi na habari za uhakika ni kwamba wahusika hao wote wamepokea na leo Jumatano wanaanza kufanyia kazi.

Yanga inayowakilishwa na jopo la mawakili watano wakiwemo Juma Nassoro, Alex Mgongolwa,Simon Patrick,Kalaghe Rashid na Respicius Didace inataka kupewa pointi tatu kwenye mchezo huo uliokuwa upigwe Machi 8,2025 lakini pia ikitaka kuchukuliwa hatua kwa maafisa ya TFF na TPLB ambao waliuharisha mchezo huo.

Kabla ya CAS kujiridhisha mawakili hao wa Yanga walikuwa na wiki mbili ngumu wakitakiwa kuwasilisha nyaraka mbalimbali za mashtaka yao ambapo baada ya uwasilishaji huo mahakama hiyo imeona mashiko na kuamua kuendelea.

Endapo CAS isingejiridhisha kupitia vielelezo vya Yanga shauri hilo lingeishia mezani lakini mambo yameonekana kuwa tofauti na sasa kesi hiyo inasonga mbele.

Hatua hiyo ya CAS kuzipa nafasi TFF, TPLB na Simba kutuma utetezi wao inakuja baada ya mahakama hiyo ya maamuzi ya juu ya michezo kujiridhisha kwamba malalamiko ya Yanga yana mashiko.

Baada ya Simba, TPLB na TFF kuwasilisha vielelezo vyao CAS wakipewa siku 10 za uwasilishaji ambapo kwanza washtakiwa watapokea nakala ya malalamiko ya Yanga ili wajibu.

Hatua itakayofuata ni CAS kupanga jaji wa kusikiliza shauri hilo huku pande zote nne zitatakiwa kushirikiana kuchangia gharama za kusikilizwa kwa kesi hiyo ambazo ni zaidi ya Sh60Milioni.

Hata hivyo endapo TFF,TPLB na Simba zitagoma kulipa gharama na Yanga kulipa gharama hizo Mwanaspoti linafahamu kwamba mlalamikaji atatakiwa kubeba mzigo huo.

Mkurugenzi wa Sheria wa TFF Boniface Wambura amekiri kupokea barua pepe hiyo ya CAS ambapo haraka wataanza kuifanyia kazi.

“Nikweli tumepokea hiyo barua ya CAS, tupo kwenye mapumziko ya sikukuu ya Eid lakini nadhani kuanzia kesho TFF itaanza kuifanyia kazi kuwasilisha yale yote watakayoyahitaji,”alisema Wambura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *