Dar es Salaam. Wiki hii kumeibuka tetesi za staa wa Bongo Fleva, Aslay Isihaka inadaiwa ana mpango wa kujiunga na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Kutokana na stori hizo zinazotawala mitandao ya kijamii hasa baada ya kuibuka pia kwa tetesi za kuondoka kwa msanii mwingine Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mboso’, Mwananchi liliamua kumtafuta Aslay ili athibitishe tetesi hizo.
Hata hivyo, mkali huyo wa nyimbo kama ‘Natamba’, Naenjoy’, ‘Pusha’, ‘Mhudumu’ na nyingine nyingi ameonyesha kupata kigugumizi juu ya tetesi hizo.
Aslay amesema yupo tayari kufanya kazi WCB, ila kwa habari anazohusishwa nazo kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kujiunga nao, hawezi kuzizungumzia sababu yuko bize na kuandaa albamu yake anayotegemea kuiachia ikikamilika.

Ilivyokuwa
Mwananchi lilimpigia simu na inaonekana alikuwa studio akirekodi nyimbo zake na alipoulizwa kuhusu tetesi hizo alijibu;
“Sister vipi? Niko bize hapa kuandaa albamu yangu nikimaliza nakupigia tuyajenge, ila kuhusu hizo habari sio wakati wake wa kuzungumzia hapa.”
Hata hivyo, Mwananchi halikukata tamaa kujua ukweli wa endapo ataenda kwenye lebo hiyo na lilimuuliza kama ikitokea anahitajika kujiunga WCB anaweza kukubali?
“Sina shaka na kujiunga na WCB, niko tayari, mimi bado kijana naendelea kutafuta pesa, pia ni msanii ninayeweza kufanya kazi na yeyote au kampuni yoyote ile cha muhimu ni kuelewana pande zote mbili.”
Vipi lebo aliyoko?
Mwananchi lilimuuliza kuhusu lebo ya muziki aliyoko sasa ya Sony Music Entertainment Africa inayosimamiwa na Seven Mosha endapo atavunja nayo mkataba au ni namna gani ataondoka.
Hata hivyo, alisema inaweza kumruhusu kufanya kazi na lebo nyingine na kinachoangaliwa ni masilahi.
“Kampuni yangu haina tatizo kinachoingaliwa ni kuingiza pesa.”

Msikie Seven
Kwa upande wake, Seven ambaye ni mkuu wa lebo hiyo Afrika Mashariki na msimamizi wa kazi za Aslay amesema habari za msanii huyo kujiunga na WCB wamezisikia ila wao hawamzuii kwani kazi ya lebo yao ni kusambaza kazi za wasanii.
“Hizo habari sisi tunazisikia tu za Aslay, ila tunachojua hadi sasa yupo kazini na anaendelea kufanya kazi zake za muziki kama kawaida, kama ikitokea hivyo kwenda WCB atatujulisha kwani tupo kwa ajili ya kusambaza kazi zake na sio kummeneji yeye.”

Meneja abariki
Yusuph Chambuso aliyewahi kuwa meneja wa Aslay amesema, kama habari za Aslay kujiunga na WCB ni za kweli, basi anampa baraka zote.
“Mimi hizi habari za Aslay nimezisikia tu kama ulivyozisikia wewe, sababu sasa hivi sipo na Aslay ila huwa nawasiliana naye sana, ila nina kama miezi kadhaa sijawasiliana naye, hivyo sijui chochote na kama kweli hizi habari zilizipo kwenye mitandao kuhusu kujiunga WCB mimi naona sawa tu nampa baraka zote, kikubwa ni makubaliano ya utendaji wa kazi,” amesema Chambuso
Hii si mara ya kwanza kwa Aslay kuhusishwa na habari za kujiunga na lebo hiyo na wakati akiwa na bendi ya Yamoto, ilipovunjika ilidaiwa anahamia huko kutokana na kutoa nyimbo zake mfululizo.
Baada ya kutoa nyimbo hizo, alikaa kimya kwa muda na hapo ndipo zilipoibuka tetesi za kwenda Wasafi ingawa alikanusha. Hata hivyo, ikumbukwe, aliwahi kuweka wazi kuhusu uwezekano wa kufanya kolabo na Diamond kama nafasi itatokea.