Ishu ya Ally Kamwe yaibua mitazamo tofauti

Wanasheria wamekuwa na mitazamo tofauti katika sakata la kukamatwa Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe huku wakigusia kilichowahi kutokea Mkuu wa Idara ya Habari wa Simba kwa Ahmed Ally.

Maofisa habari hao kwa nyakati tofauti, wameingia kwenye sintofahamu na wakuu wa mikoa ya Mwanza, Said Mtanda na Paul Chacha wa Tabora huku Bodi ya Ligi ikionya utani wa mpira uliopitiliza.

Hata hivyo, wanasheria wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu sakata la maofisa habari hao, hususani la Kamwe, ambaye alilala ‘korokoroni’ baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Tabora.

Kamwe alikamatwa Aprili 2, 2025 saa 7 usiku mkoani humo kabla ya jana saa 5 asubuhi Kamanda wa Polisi Tabora,  Richard Abwao kulithibitishia Mwananchi kuwa wanamshikilia Kamwe kwa kutoa kauli chafu kwa viongozi wa Serikali hata hivyo jioni iliripotiwa kuwa ameachiwa huru.

Kushikiliwa kwa Kamwe kumeibua mitazamo tofauti,  baadhi ya wanasheria wakidai hana kosa kwa kuwa kisheria hakuna kosa la kutoa kauli chafu kwa viongozi wa Serikali na kudai hata kama alitoa pia alikuwa katika utani wa mpira huku wengine wakisema kosa la jinai halijalishi limefanyika katika mazingira gani, sheria iko palepale.

Kamwe alishikiliwa ikiwa ni saa kadhaa zimepita tangu arushe dongo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha katika hamasa kuelekea mchezo wao dhidi ya Tabora United uliomalizika  Aprili 2, 2025 kwa Yanga kushinda mabao 3-0.

Katika video iliyosambaa mitandaoni inamuonyesha Kamwe akiwa mkoani Tabora akifanya hamasa ya mchezo huo huku akisema: “Kuna watu wanatafuta kiki..mkuu wa mkoa nani huyu, Chacha eenh? atachacha kweli baada ya mechi,”

Hiyo ilikuwa ni baada ya mkuu wa mkoa huyo kuiahidi Tabora United endapo itamfunga Yanga itapewa bonansi ya Sh60 milioni.

Tukio hilo na lile la Novemba 21, 2024, la Ahmed Ally kutofautiana na mkuu wa mkoa wa Mwanza, Said Mtanda yameibua mitazamo tofauti ya kisheria.

Katika tukio la Mwanza, mpiga picha wa Simba, Rabbi Hume alichapisha kipande cha video kwenye ukurasa wake wa Instagram kikionyesha mvutano wa watu kwenye geti kuu la kuingia ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba, vurugu hizo zikitajwa kuwa ni viongozi wa Simba wanakamatwa na watu aliodai wametumwa na RC Mtanda.

Klabu ya Simba ilitoa taarifa kwa umma ikilaani kitendo cha RC Mtanda kuvamia mazoezi ya mwisho ya timu yao na kuwakamata Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu na Kocha Msaidizi, Seleman Matola.

Hata hivyo, Mtanda alikanusha madai hayo, akiziita tuhuma hizo ni propaganda zinazosambazwa kutuliza upepo wa mchezo wa Pamba Jiji dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mtanda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo alieleza kuwa mwathiriwa wa kitendo hicho kwa kuwa ni mlezi wa Pamba Jiji na kudokeza kumsamehe Ahmed Ally baada ya kudai ofisa habari huyo wa Simba alimchafua.

Mitazamo ya Kisheria

Matukio haya mawili yamekuwa na mitazamo tofauti, baadhi ya mawakili wakiwakingia vifua Ally na Kamwe na kutaka wakuu wa mikoa, wasijiingize kwenye ushabiki wa mpira kama watashindwa kujivua madaraka.

Hata hivyo wengine wanasema tukio lolote la jinai linapofanyika katika mazingira yoyote, iwe hata ya mpira, haiwezi kuiondoa hiyo jinai.

Wakili Kiongozi wa kampuni ya uwakili ya Haki Kwanza, Aloyce Komba amesema kwa sababu ambazo RPC Abwao ameitaja ya kumshikilia Kamwe kwa kutoa kauli chafu kwa viongozi wa Serikali, si kosa kisheria.

“Bado sisi hatujui Kamwe amekamatwa kwa kosa gani? polisi haijasema aliyefungua RB polisi ni nani na mlalamikaji ni nani? lakini kama ni kosa ni kuwatolea lugha chafu viongozi wa Serikali, katika sheria hakuna kifungu cha namna hiyo,” amesema Komba na kuhoji.

“Polisi iseme hiyo lugha chafu ni lugha gani? mlalamikaji ni nani na iseme ‘charge sheet’ ni hii, mfano unaposema tumemkamata kwa tuhuma za za kujeruhi, kuiba, kumtukana mkuu wa mkoa na matusi ni haya na haya,”.

Akigusia kauli ya utani ambayo aliitoa Kamwe kabla ya mechi hiyo, Komba amesema alivyomsikia wakati wa hamasa ya mechi ya Yanga na Tabora alisema,” kuna mtu kaja amevaa shati lake la ubatizo, ameahidi milioni 60 ambazo sisi pesa hizo tunazitumia kulia pilau na Wanayanga wa Tabora,”.

“Labda wangesema amemkejeli mkuu wa mkoa, suala hilo pia lingekwenda kwenye maadili, lakini katika sheria ya makosa ya jinai, bado sioni kosa la Kamwe,” amesema

“Hata hivyo kitu mbacho tunapaswa kukifahamu, inapotokea mechi kama hizi basi, wakuu wa mikoa wasiingie kwenye ushabiki.

“Ukiingia  huko basi uvue ukuu wa mkoa, uenyikiti wa ulinzi na usalama ukae pembeni ubaki kama shabiki mwingine yoyote, kwenye mpira unapoingia kwenye utani, cheo, madaraka unaweza pembeni huko kuna maumivu ya kufungwa na kutaniwa,” amesema Komba.

Wakili Omary Msemo amekuwa na mtazamo tofauti akibainisha, sheria ni sheria na haisemi ulichokifanya ni kosa au si kosa, au tuhuma ulizonazo ni sahihi au si tuhuma kwa kuangalia mazingira.

“Hata ukiwa kwenye utani wa mpira, kama umefanya jinai itakuwa ni jinai, sheria yoyote ya jinai huwa haingalii upo mazingira gani,” amesema Msemo.

Japo hakugusia kwa undani sakata la Kamwe na lile la Ahmed Ally, Msemo amesema katika sheria mtu anaweza kuwa anafanya utani, lakini kauli yoyote ikileta jinai, kinachoangaliwa ni element za kosa.

“Kwenye jinai haingalii mazingira, mfano mlikuwa mnacheza ukamsukuma mwenzako akapoteza maisha, sheria haisemi ilikuwa utani, mazingira hayakulindi, isipokuwa kunaweza kupunguza vitu fulani fulani lakini haikuondoi kwenye jinai,” amesema.

Wakili Jebra Kambole amesema katika sheria hakuna kosa la kutoa lugha chafu kwa viongozi wa Serikali.

“Sheria inakataza kutoa taarifa za uongo kwa nia ya kumdhalilisha mtu, inakataza matusi, lakini hakuna kosa la kutoa lugha chafu kwa viongozi wa Serikali,” amesema.

Amesema kutoa lugha chafu kwa viongozi inaweza kuwa sio tabia nzuri, lakini sio jinai akifafanua hilo amesema pia itaangaliwa muktadha wa mazunguzo hayo.

“Wakati akitoa lugha hiyo alikuwa kama kiongozi wa Serikali au shabiki wa mpira? kwani kuna maeneo kiongozi huyo huyo anakuwa baba, anakuwa muumini kanisani, kuna sehemu atakuwa mwanafunzi, kuna sehemu utakuwa mtoto na sehemu nyingine kutokana na mazingira.

‘Kwenye ili, nadhani Serikali ijitahidi kutojihusisha moja kwa moja na masuala ya michezo, tusiingize siasa, serikali na michezo, hivi sasa kuna hii ‘trend’ ya wakuu wa mikoa kuingilia michezo, si sawa, washiriki kukuza michezo si kufanya ushabiki wa michezo,” amesema Kambole.

Mwanasaiokolojia, Deogratius Sukambi amesema katika soka kumekuwa na mgogoro baina ya ushabiki, sheria za nchi na sheria za michezo.

“Japo mimi si mtaalamu sana wa sheria, lakini kuna mgongano huo, mkuu wa mkoa kuingilia masuala ya mpira kuna dosari na ofisa habari kumuongelea mkuu wa mkoa nalo ni tatizo,” amesema Sukambi.

Bodi yaonya

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto amesema kinachotokea kwenye mivutano ya maofisa habari wa timu hizo na wakuu wa mikoa si jambo zuri.

“Kuna mambo ya kuongea kuleta hamasa ya timu, yanaruhusiwa, lakini kupitiliza huo ni utashi wa mtu, unapovuka mipaka siku zote sheria huwa inachukua mkondo wake,” amesema Mguto.

Amesema yeye Mguto haamini kama Kamwe ni msemaji wa Yanga, anachokiamini ni ofisa habari wa klabu hiyo.

“Kwa muktadha huu ili asimame aongee, kuna vitu lazima apewe na Sekretarieti ya Yanga aviongee na asipunguze wala kuongeza kitu,” amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *