Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB limeshinda tuzo maalumu ya “Uhandisi wa Utangazaji” ya Umoja wa Redio na Televisheni za nchi za Asia na Pasifiki (ABU) ya mwaka 2024.
Mtandao wa Sahab umenukuu Idara ya Mawasiliano ya Umma wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na kuripoti kuwa, katika hafla iliyofanyika siku ya Jumanne mjini Istanbul, Uturuki tuzo maalumu ya Uhandisi wa Utangazaji ya Umoja wa Redio na Televisheni za nchi za Asia na Pasifiki (ABU) limetunukiwa shirika hilo la IRIB kwa kuzindua idhaa 208 za ndani kwa ajili ya uchaguzi kupitia mtandao wa televisheni za kidijitali.
Mradi huo wa kitaifa ulizinduliwa sambamba na kukaribia kufanyika uchaguzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mnamo mwezi Machi mwaka huu, ambapo kila eneo, kati ya maeneo 208 ya uchaguzi nchini ilipatiwa idhaa ya kuendeshea kampeni za wagombea.

Mkutano Mkuu wa 61 wa ABU wa mwaka huu ulifanyika kuanzia tarehe 18 hadi 23 Oktoba katika mji wa Istanbul, Uturuki kwa kauli mbiu ya “Kuunganisha akili bandia, Utangazaji wa Vyombo vya habari na Jamii”.
Umoja wa Redio na Televisheni za nchi za Asia na Pasifiki uliasisiwa mwaka 1964 na hivi sasa ukiwa na wanachama 280 kutoka nchi 57, unahesabiwa kuwa moja ya jumuiya kubwa zaidi na ya kitaalamu zaidi ya vyombo vya habari duniani…/