Msemaji wa serikali ya Iraq amesema: Baghdad inalaani uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Iran na kwamba, nchi hiyo inatangaza mshikamano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Bassem al-Awad, msemaji wa serikali ya Iraq amesema hayo katika radiamali yake kwa hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kuubainisha kwamba, kitendo hicho ambacho ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya Iran hakikubaliki.
Msemaji wa serikali ya iraq amesisitiza katika taarifa hiyo kuwa, utawala ghasibu wa Kizayuni unaendelea na siasa zake za uhasama na upanuzi wa vita katika eneo na mashambulizi yake ya wazi bila ya vikwazo vyovyote, na mara hii umelenga shabaha za Iran.
Aidha amesema, hapo awali Iraq ilitahadharisha kuhusu matokeo hatari ya kunyamaza kimya jumuiya ya kimataifa dhidi ya mienendo ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na mashambulizi dhidi ya Lebanon na Syria na vilevile hujuma dhidi ya Iran.

Wakati huo huo, Sayyid Muqtada Sadr, Kiongozi wa harakati ya Sadr ya Iraq amesisitiza kuwa, licha ya kwamba mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, lakini ni madogo mno na hayana thamani ya kulaaniwa.
Moqtada Sadr amesema: Majibu ya Israel yalikuwa hafifu na yanaonyesha kiwango cha kuchanganyikiwa na wasi wasi mkubwa wa utawala huo na waungaji mkono wake kutokana na uthabiti wa nafasi ya Iran na ujasiri wa makundi ya muqawama huko Palestina na Lebanon.