Iraq yailalamikia Israel Umoja wa Mataifa kutumia anga yake kuishambulia Iran

Serikali ya Iraq imewasilisha malamiko yake rasmi katika UUmoja wa Mataifa kulalamikia hatua ya Israel ya kutumia anga yake kuishambulia Iran.

Leo Jumatatu, serikali ya Iraq imetangaza katika taarifa yake kuwa imewasilisha malalamiko kwenye Umoja wa Mataifa kupinga kitendo cha utawala haramu wa Israel cha kutumia anga yake kuishambulia Iran.

Katika malalamiko yake yaliyowasilishwa kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Iraq imelaani vikali hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kutuumia anga yake kuishambulia Iran.

Katika taarifa yake, Iraq ilieleza hatua ya Israel kama “ukiukaji wa wazi wa anga na mamlaka ya Iraq”.

Juzi Msemaji wa serikali ya Iraq alisema: Baghdad inalaani uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Iran na kwamba, nchi hiyo inatangaza mshikamano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alikuwa ameomba kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kuhusu shambulio la Israel dhidi ya Iran katika barua aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Amesisitiza kuwa Tehran “inahifadhi” haki ya kujibu mashambulizi ya Israel. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano leo kujadili mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran.