Iran yatoa onyo: Marekani inahatarisha maisha ya askari wake kwa kuwapeleka Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi ameionya Marekani dhidi ya kupeleka wanajeshi wake Israel kwa ajili ya kuendesha mitambo yake ya kutungulia makombora, akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haina “mistari myekundu” katika kulinda maslahi yake.

Araghchi ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kufuatia habari kwamba Marekani imeamua kuupelekea utawala wa Kizayuni wa Israel mtambo wa kutungulia makombora wa Terminal High Altitude Area Defence (THAAD) ambao utahitaji kutumwa pia wanajeshi wa Marekani kwa ajili ya kuuendesha.

Araghchi amebainisha kuwa Washington imekuwa ikituma kiwango kisicho na idadi cha silaha kwa Israel wakati wa vita vyake dhidi ya Ukanda wa Ghaza uliozingirwa, na akaongezea kwa kusema, sasa “inaweka maisha ya wanajeshi wake hatarini” kwa kuwapeleka Israel ili kuendesha mitambo ya makombora ya Marekani.

Mtambo wa THAAD

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kwa kusema: “ingawa tumefanya juhudi kubwa katika siku za hivi karibuni kudhibiti vita vya pande zote katika kanda yetu, (lakini) nasema wazi kwamba hatuna mistari myekundu katika kulinda watu wetu na maslahi yetu.”

Hayo yanajiri huku msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon Meja Jenerali Pat Ryder akithibitisha kuwa, kufuatia agizo lililotolewa na rais wa nchi hiyo na kuidhinishwa na waziri wake wa ulinzi, Washington inapeleka Israel mtambo wa kutungulia makombora wa THAAD pamoja na wafanyakazi wa kuuendesha ili kusaidia kuimarisha ulinzi wa anga wa utawala huo wa Kizayuni kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi yake Aprili 13 na baadaye Oktoba Mosi mwaka huu.

Wataalamu wa masuala ya kijeshi wameitafsiri hatua hiyo ya Marekani kuwa ni uthibitisho kamili wa kushindwa mtambo unaosifika wa kutungulia makombora wa Israel wa Kuba la Chuma (Iron Dome) kukabiliana na makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, bali hata ya vikosi vya Muqawama katika eneo…/