
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametilia mkazo wajibu wa kushirikiana jamii zote duniani katika kuhakikisha utawala wa Kizayuni wa Israel unakomesha jinai zake huko Palestina na Lebanon.
Sayyid Abbas Arghchi alisema hayo jana wakati alipoonana na kuzungumza na Elmedin Konaković, waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Bosnia Herzegovina pambizoni mwa Kikao cha Kumi cha Baraza la Umoja wa Mataifa la Muungano wa Tamaduni nchini Ureno na kusema kuwa, jamii ya wanadamu duniani ina wajibu wa kutekeleza jukumu lake la kushirikiana ili kukomesha jinai za utawala ghasibu wa Israel huko Palestina na Lebanon.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia jinsi Jamhuri ya Kiislamu inavyolipa umuhimu mkubwa suala la ushirikiano baina ya nchi za dunia na hasa za Kiislamu na kusema kuwa, Tehran iko tayari kuimarisha zaidi uhusiano wake na Bosnia na Herzegovina katika masuala ya pande mbili na ya kimataifa.
Amesema hali katika eneo la Asia magharibi ni ya hatari sana hivi sasa kutokana na jinai na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala katili wa Kizayuni huko Lebanon na Palestina na kusema kuwa, nchi zote za dunia zinazoshiriki katika jinai za Israel zina dhima ya maafa yanayotokea Palestina na Lebanon na kwamba kila nchi ulimwenguni ina wajibu wa kufanya juhudi za kukomesha jinai hizo za utawala wa Kizayuni.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Bosnia Herzegovina amezungumzia nafasi muhimu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi hasa katika kulinda usalama na utulivu wa eneo hilo na ametaka ushirikiano zaidi uwepo ili kuzuia kuenea hatari za kiuslama duniani.