
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumza kwa simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Ufaransa na kuonya kuhusu matokeo mabaya na hatari mno ya chokochoko mpya za utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi.
Sayyid Abbas Araghchi ametoa onyo hilo kali kwenye mazungumzo ya simu na Waziri Mambo ya Nje wa Ufraransa, Jean-Noël Barrot wakati pande mbili zilipobadilisha mawazo kuhusu hali halisi iliyopo hivi sasa kwenye eneo hili.
Katika mazungumzo hayo, Araghchi ametilia mkazo wajibu wa kukomeshwa mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni huko Palestina na Lebanon na kusisitiza kuwa chokochoko hizo mpya za Wazayuni zitalitumbukiza eneo hili na dunia nzima katika hatari kubwa isiyofidika.
Amezungumzia pia hali mbaya ya wakimbizi wa Palestina na Lebanon na kuitaka jamii ya kimataifa iilazimishe Israel iruhusu mashirika ya misaada ya kibinadamu kuwafikia wakimbizi hao.
Katika kipindi cha siku za hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo kadhaa ya simu na viongozi wa nchi za Ulaya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mara zote amekuwa akionya kuhusu chokochoko mpya za utawala wa Kizayuni.
Muda wote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaonya kwamba, shambulio lolote dhidi yake litajibiwa vikali. Pamoja na hayo, mara zote Tehran imekuwa ikisema kwamba siasa zake kuu na za muda wote ni kuepusha vita na mivutano lakini wakati huo huo imejiandaa kikamilifu kulinda haki zake na kutoa majibu yasiyotabirika kwa mvamizi yeyote yule.