Iran yaonya kuhusu azimio lolote dhidi ya Tehran katika kikao cha Bodi ya Magavana wa IAEA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametangaza kuwa hatua yoyote dhidi ya Tehran katika kikao kijacho cha Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) itazidisha ugumu wa hali ya kurekebisha hali ya kuzalisha nishati ya nyuklia yenye malengo ya amani ya Jamhuri ya Kiislamu.

Abbas Araqchi ametoa matamshi hayo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, leo Jumatano wakibadilishana mawazo kuhusu mazungumzo ya nyuklia na matukio ya hivi karibuni ya kikanda.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amelaani vikwazo vipya vya Ulaya dhidi ya mashirika ya ndege na meli ya nchi hiyo akivitaja kuwa ni hatua “isiyo ya haki na ya uchochezi” kwa kile kilichodaiwa kuwa Tehran ni inatuma zana za kijeshi kwa Moscow ili kutumika katika vita vya Ukraine.

Araqchi pia amekemea vikali uamuzi wa nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kuwasilisha azimio dhidi ya Iran katika kikao cha Bodi ya Magavana wa IAEA leo Jumatano.

“Hatua hii ya nchi tatu za Ulaya inakiuka waziwazi mazingira chanya yaliyoundwa katika mahusiano kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kuongeza kuwa “Itafanya mambo kuwa magumu zaidi.”

Akiashiria matukio ya kieneo na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya Lebanon na vilevile mauaji ya kimbari ya utawala huo ghasibu huko Gaza, Araqchi amelaani uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa jinai za Tel Aviv na kutaka hatua za dharura zichukuliwe na pande zenye ushawishi ili kuilazimisha Israel kusimamisha mauaji hayo.