
Balozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameliandikia barua Baraza la Usalama la Umoja huo na kulitaka litoe azimio la kulaani shambulio la kigaidi la genge linalojiita “Jeysh al Adl” katika mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran.
Baada ya kushindwa utawala katili wa Kizayuni kukabiliana na kambi ya Muqawama, na kufeli shambulio lake la kigaidi katika baadhi ya maeneo ya Iran, genge lililolaaniwa linalojiita “Jeysh al Adl” Jumamosi ya Oktoba 26, 2024 lilifanya shambulio la kigaidi na kuua kidhulma askari polisi 10 wa Iran katika mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa nchi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la ISNA, Amir Saeid Iravani, Balozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza Kuu la umoja huo akitaka kutolewe azimio la kulaani jinai hiyo ya magaidi wanaoungwa mkono na madola ya kibeberu wanaoendesha vitendo vya kigaidi dhidi ya wananchi na maafisa usalama wa Iran.
Mbali na kutaka kutolewe azimio hilo na Umoja wa Mataifa, Balozi Iravani ametaka pia barua alizowaandikia viongozi hao wakuu wa umoja huo zisajiliwe kama ushahidi ndani ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu kama kinavyosema kifungu nambari 110 cha utendaji kazi za umoja huo ambacho kinahusiana na wajibu wa kuchukuliwa tadibiri madhubuti za kung’oa kabisa vitendo vya kigaidi.