Iran yalaani mpango wa kibaguzi na kitanuzi wa Israel wa kunyakua Ukingo wa Magharibi

Iran imelaani vikali wito wa waziri mmoja wa utawala haramu wa Israel wa kunyakua kikamilifu eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi ambalo hivi sasa linakaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema jana Jumatano kwamba mpango huo ni dalili nyingine ya “tabia ya kibaguzi, kujitanua na mbinu ya uchokozi” ya utawala wa Israel.

Baghaei ametoa taarifa hiyo kufuatia matamshi ya Novemba 11 ya waziri wa fedha wa Israel Bezalel Smotrich.

Smotrich alisema ameagiza maandalizi ya kunyakuliwa kwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa matumaini kwamba utawala wa Israel utapata mamlaka kamili katika eneo hilo mnamo 2025.

Msemaji huyo wa Iran amesema utawala wa Kizayuni hunyakua ardhi za a Palestina kila mara kama sehemu ya mpango wa kuiangamiza Palestina kikamilifu. Amesema mpango huo umekuwa ukitekelezwa kwa njia ya kikatili zaidi katika mwaka uliopita.

Baghaei amesisitiza wajibu wa kisheria na kimaadili wa serikali zote zinazohusika kuzuia na kuadhibu wahusika wa mauaji ya kimbari na kukabiliana na uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu.

Ameelezea masikitiko yake makubwa juu ya juhudi za Marekani na Ujerumani za kuzuia njia ya kuwawajibisha viongozi wa Israel na kuwafikisha mahakamani katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Afisa huyo wa Iran ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti na jamii ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kukomesha mauaji ya kimbari huko Palestina na uchochezi wa utawala huo ghasibu huko Lebanon na Asia Magharibi.

Amesema juhudi hizo za mauaji ya kimbari kamwe haziwezi kudhoofisha nia ya wananchi wa Palestina na azma yao ya kuzikomboa ardhi zao.