Iran yakanusha madai ya kuhusika katika mauaji ya kuhani wa Israel huko Abu Dhabi

Ubalozi wa Iran mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umepinga madai ya kuhusika kwa namna yoyote na mauaji ya kuhani wa Kizayuni mjini Abu Dhabi.

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel viliripoti jana Jumapili kwamba mwili wa kuhani wa Kizayuni, Zvi Kogan aliyekuwa ametoweka tangu Alkhamisi iliyopita, umepatikana huko Imarati.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya UAE ilitangaza katika taarifa yake Jumapili usiku kwamba imewakamata wahusika watatu wa mauaji ya Kogan.

Kufuatia mauaji ya Rabi wa Kizayuni, Zvi Kogan huko Imarati, baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel viliituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa imehusika katika mauaji hayo.

Kwa msingi huo taarifa ya ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Imarati imesema: “Tunapinga kikamilifu madai kwamba Iran imehusika kati mauaji ya kuhani huyo.”

Mapema leo pia gazeti la Yedioth Ahronoth la Israel limenukuu vyanzo vya utawala huo kwamba ushahidi unaonyesha kwamba waliohusika na mauaji ya rabi huyo wa Israel hawakuchukua hatua kwa maelekezo ya Iran.

Baadhi ya vyombo vya habari vinasema kuhani Zvi Kogan ameshirika katika mauaji ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Kuhani huyo ni moja ya wanachama kundi  lenye misimamo mikali la The Chabad Movement ambalo linapinga haki ya kuwepo Wapalestina, na linataka wafukuzwe kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Kundi hilo pia linapinga makubaliano yoyote yanayoweza kuwapa Wapalestina sehemu ya ardhi ya Palestina.