Iran yaionya Marekani kuhusu kukariri siasa zilizofeli za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani dhidi ya kuanzisha tena kampeni yake ya “mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa” dhidi ya Tehran na kusisitiza kwamba, majaribio ya hapo awali ya Washington ya kuishinikiza Iran yalishindwa na kugonga mwamba.

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, aliyasema hayo katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumanne na kubainisha kwamba: ‘Toleo la kwanza la mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa lilikabiliwa na upinzani wa kiwango cha juu kabisa wa Tehran, na kuifanya Washington ishindwe kwa kiwango cha juu kabisa.’ Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewashauri viongozi wa Marekani kujaribu kutekeleza wazo la “mantiki ya juu kabisa” kwa sababu ni kwa manufaa ya pande zote. Araghchi amehoji, je, mnataka ushahidi? Kama mfano mdogo tu, linganisheni hali ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran kabla na baada ya siasa zinazodaiwa kuwa za “mashinikizo ya juu kabisa”. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika zaidi kwamba jaribio la kutumia “toleo la pili la mashinikizo ya juu kabisa” litapelekea tu kufikiwa “toleo la pili la Marekani kushindwa kwa kiwango cha juu kabisa.”

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kutofaulu kwa hatua za upande mmoja na vikwazo dhidi ya Iran, viongozi wa Marekani wangali wanaendeleza siasa zao za kuibua mvutano nchini Iran kupitia vikwazo. Vikwazo hivyo ambavyo vinatekelezwa kwa lengo la kuharibu uchumi wa Iran, kinyume na matarajio ya Ikulu ya White House, vimepelekea serikali na wananchi wa Iran wasimame kidete pamoja dhidi ya siasa hizo za chuki dhidi yao.

Utawala wa Rais Joe Biden na chama cha Democrats unaendeleza siasa zile zile za chuki za serikali zilizopita za Marekani dhidi ya taifa la Iran. Ni wazi kwamba hata kama Kamela Harris, makamu wa rais wa sasa wa Biden na mgombea aliyeshindwa wa Democrats katika uchaguzi wa hivi karibuni wa rais wa nchi hiyo, angeshinda, bado angeendeleza mchakato ule ule wa uadui wa Marekani unaopigiwa debe hivi sasa na Donald Trump dhidi ya Iran.

Vitendo vinavyoibua mvutano vya viongozi wa Marekani havitakuwa na matokeo mengine kwa mustakabali wa Marekani isipokuwa kuongeza mashinikizo ya ndani na migawanyiko ya kijamii katika nchi hiyo. Utendaji wa viongozi wa Marekani katika vita vya Ukanda wa Gaza na uungaji mkono wao wa kila upande kwa utawala wa Kizayuni umepunguza uungaji mkono na kuongeza kuchukiwa nchi hiyo katika ngazi za kieneo na kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Palestina na muqawama umekuwa na taathira chanya katika nchi za Kiislamu na waungaji mkono wa Palestina katika ngazi za kimataifa.

Siasa za “mashinikizo ya juu kabisa” zimetokana na dhana potovu ya viongozi wa Marekani kwamba huenda ongezeko la vikwazo vya kiuchumi vinavyojumuisha sekta ya afya vikailazimisha Iran kubadilisha siasa zake katika eneo. Hata hivyo, matukio ya kisiasa katika miaka michache iliyopita yamethibitisha wazi kwamba hatua kama hizo zinazotekelezwa na watawala wa Marekani dhidi ya Iran hazijakuwa na matokeo yaliyokusudiwa, ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wa pili inaendelea kupiga hatua kubwa na za haraka kimaendeleao katika sekta ya sayansi na tejnolojia, hususan kuhusu nishati ya nyuklia. Kurushwa kwa satelaiti mbalimbali za kisayansi, kiuchunguzi na kijeshi katika anga za mbali pia kumethibitisha ukweli kwamba viongozi wa Iran hawatachelewesha maendeleo ya nchi kwa msingi wa ahadi tupu zinazotolewa na Marekani au nchi nyingine za Magharibi.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imechukua hatua muhimu katika kupunguza mashinikizo ya vikwazo ambapo imeunda mtandao madhubuti wa kukwepa vikwazo hivyo, na kwa hivyo, duru ya pili ya mashinikizo ya juu kabisa itakabiliwa na matatizo makubwa zaidi kuliko ilivyokuwa duru ya kwanza. Kuongezeka kwa mauzo ya mafuta, biashara za nje, kiwango cha biashara na nchi jirani, uanachama wa Iran katika jumuiya kama vile BRICS na Shanghai ni miongoni mwa hatua ambazo Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran imezichukua kwa ajili ya kupunguza athari za vikwazo hivyo vya kidhalimu dhidi yake.

Vikwazo vya nchi za Magharibi vilivyofeli dhidi ya Iran

“Mradi na ndoto ya mapinduzi”, ambayo imekaririwa mara kwa mara na baadhi ya matabaka ya kisiasa yenye mafungamano na Wazayuni nchini Marekani ambapo viongozi wa Washington wametakiwa kuitekeleza, imeshindwa kabisa, na hilo linatokana na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kabla ya kuingia tena Ikulu ya White House, Trump pia amekiri ukweli kwamba kutokana na matatizo ya ndani ya Marekani, nchi hiyo haina nia ya kufuatilia ndoto hiyo ya eti kubadilisha serikali ya Iran na kuwa iko tayari kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran kuhusu masuala tofauti. Ni wazi kwamba, kutekelezwa madai hayo kunahitajia mabadiliko ya msingi katika siasa za kiadui za Ikulu ya Marekani dhidi ya Iran, siasa ambazo hazijasitishwa katika miaka ya hivi karibuni.

Kujitoa katika mapatano ya JCPOA ni moja ya uvunjaji ahadi wa Marekani kwa Iran, na ni wazi kwamba, madai na ahadi za uongo za viongozi wa Marekani haziwezi kutegemewa bila ya kuwepo nia ya kivitendo ya kurekebisha siasa hizo zilizofeli huko nyuma. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amewashauri viongozi wa Marekani kufuata siasa za mantiki ya kiwango cha juu kabisa, siasa ambazo matokeo yake yana madhara madogo kwa Marekani yenyewe.