Iran yaadhimisha Siku ya Kitaifa ya Mashujaa, kwa heshima ya Shahidi Qassem Soleimani

Iran leo inaadhimisha Siku ya Kitaifa ya Mashujaa , ikitoa heshima kwa mmoja wa watu wake wakuu, Shahidi Qassem Soleimani.

Siku hii inaadhimisha kumbukumbu ya barua yake ya kutangaza kushindwa kwa kundi la kigaidi la Daesh au ISIS, nukta inayoashiria dhamira thabiti ya Iran ya kupinga ubeberu na ugaidi.

Katika barua mashuhuri ya tarehe 21 Novemba 2017, kamanda mashuhuri wa kupambana na ugaidi wa Iran Luteni Jenerali Qassem Soleimani alitangaza kushindwa Daesh, kundi la kigaidi ambalo kwa muda wa miaka kadhaa lilikuwa limeteka maeneo kadhaa ya Iraq na Syria na kueneza machafuko kote Asia Magharibi.

Barua hiyo ilitumwa kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, na kutangaza kwamba “dhoruba kali” iliyoupata ulimwengu wa Kiislamu imekwisha.

Ili kuenzi mafanikio hayo makubwa, Iran iliteua rasmi Novemba 21 kama ” Siku ya Kitaifa ya Mashujaa ” mwaka jana, ikienzi nafasi muhimu ya kamanda huyo wa kupambana na ugaidi katika kumaliza sura ya giza katika eneo na kuashiria moja ya michango yake mikubwa kwa amani na utulivu wa kikanda.

Mashahidi Soleimani na Abu Mahdi Muhandis

Daesh, ambayo pia inajulikana kama ISIS au ISIL, iliibuka kutoka kwenye mabaki ya kundi la kigaidi la al-Qaeda nchini Iraq (AQI), baada ya uvamizi wa 2003 wa Marekani na kuikalia kwa mabavu Iraq.

La kusikitisha ni kuwa, maisha ya Jenerali Soleimani yalikatizwa Januari 3, 2020, katika shambulio la kigaidi la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Baghdad miaka miwili baada ya tangazo lake hilo la kihistoria.

Abu Mahdi al-Muhandis, kamanda mashuhuri wa muqawama nchini Iraq, ambaye alichukua nafasi muhimu katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi, pia aliuawa shahidi pamoja na Shahidi Soleimani.

Licha ya hasara hii kubwa na isiyoweza kufidiwa, urithi wa Jenerali Soleimani ungali unadumu, ukiadhimishwa na mamilioni wanaomchukulia kama nembo ya mapambano na amani katika eneo la Asia Magharibi.