Iran: Umoja wa Ulaya unapendelea maslahi yake kuliko sheria za kimataifa

Katika kujibu kauli ya Umoja wa Ulaya kufuatia uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Iran, ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Brussels umesema kuwa umoja huo unapendelea zaidi maslahi yake binafsi kuliko sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa kanali ya Sahab, Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Brussels umechapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X  Twitter ya zamani  kwamba; ‘Msimamo wa Umoja wa Ulaya ni dhaifu sana katika kulaani mashambulizi ya utawala dhalimu  wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran.’

Ujumbe huo umeongeza kuwa, msimamo huo unaonyesha kwamba Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake zinapendelea maslahi yao ya muda mfupi badala ya kuzingatia sheria za kimataifa na kile kinachoitwa mfumo wa sheria.

Kabla ya hapo Umoja wa Ulaya ulitoa tamko bila ya kulaani kitendo cha kichokozi cha utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran na kutaka pande zote mbili zijizuie kuchukua hatua zaidi ili kuzuia kushadidi mivutano katika eneo.

Ikumbukwe kuwa siku ya Jumamosi asubuhi, katika hatua ya kichokozi, utawala wa Kizayuni ulishambulia baadhi ya vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam, ambapo uchokozi huo ulikabiliwa na kuzimwa na mfumo jumuishi wa ulinzi wa anga wa Iran. Mfumo huo ulifanya kazi kwa mafanikio makubwa na kuzima shambulio hilo la kichokozi la Wazayuni.

Kwa mujibu wa tangazo la kijeshi ni uharibifu mdogo tu ndio ulisababishwa katika baadhi ya maeneo na uchunguzi unaendelea kufanywa kubaini uzito wa tukio hilo.