
Matibabu yasiyopatikana, kupanda kwa bei na ulanguzi wa dawa za kulevya: inazidi kuwa vigumu kupata matibabu nchini Iran. Madaktari na wafamasia wanaonya juu ya hali ambayo imekuwa ikiendelea kwa zaidi ya miaka saba na inazidi kuwa mbaya.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Nimekuwa nikitafuta doxepin kwa siku tatu na sijapata,” anasema Mona, mwanasaikolojia wa watoto. “Hali inatisha sana, kuna seramu chache (…) hatuwezi tena kupata asidi ya mefenamic kutibu maumivu ya meno au maumivu yanayohusiana na mzunguko wa hedhi,” anasema mwanamke huyu wa Iran.
Kuendelea kuporomoka kwa sarafu ya Iran dhidi ya fedha za kigeni na kusababisha mfumuko wa bei kumezidisha mzozo wa kiuchumi nchini humo na kusababisha kudorora kwa sekta ya dawa. Baadhi ya dawa haziagizwi tena: “Katika miaka ya hivi karibuni, mara nyingi imetokea kwamba baadhi ya dawa hupotea sokoni ghafla na kuwalazimisha wanaozitumia kuzibadilisha na zile wanazopata sokoni, ” anasema Reza*, daktari huko Tehran.
Uhaba wa dawa, hata vyombo vya habari vinavyo chini ya mamlaka ya serikali vinalazimishwa na wananchi kulizungumzia suala hilo. Mnamo Machi 2, 2025, shirika la habari la IRNA lilitoa nafasi kwa wagonjwa katika mkoa wa magharibi wa Chaharmahal na Bakhtiari ambao walikuwa na wasiwasi wa kutopata dawa walizohitaji. Siku mbili baadaye, chombo kingine cha habari, Mehr News, kiliangazia matokeo ya uhaba huu kwa wagonjwa wa thalassemia, ugonjwa wa damu unaohitaji kuongeza damu mara kwa mara na dawa zinazotumiwa hadi kufa.
Leila*, ambaye ana duka la dawa huko Shiraz (kusini-magharibi), anasema mgogoro huu ulianza takriban miaka saba: “Tangu 2018, pamoja na kupanda kwa ghafla kwa bei ya dola, tumekuwa tukikabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa. Hasa yale yanayohusiana na magonjwa maalum kama vile sclerosis na kisukari. Pia hatuna dawa za kimsingi kama vile albumin, ambayo ni muhimu sana kwa wale ambao wamepandikizwa au waliolazwa hospitalini. Wagonjwa wengi kwa hiyo wanalazimika kutafuta dawa zao wenyewe kwenye soko la nje, ambapo kimsingi, ni hospitali ambayo inapaswa kuwapatia,” anaelezea.
Kutokana na mfadhaiko wa wateja wake, Leila anajihisi mnyonge. Anajuta kutoweza kuwatuliza au kuwasaidia: “Wengine wananiambia ni kwa ajili ya mtoto wao, kaka yao, mama yao… naona huzuni machoni mwao na siwezi kufanya lolote,” anasema.
Kupanda kwa bei ya dawa
Katika mitandao ya kijamii, watumiaji wengi wa mtandao nchini Iran pia wamekasirishwa na ongezeko kubwa la bei ya dawa.
Mnamo Januari 26, shirika la habari la IRNA lilichapisha makala yenye kichwa cha kusisimua: “Mshtuko kutokana na kupanda kwa bei ya dawa: Wateja watatu kati ya 10 wa maduka ya dawa hawanunui dawa zao kutokana na bei kupanda.” Aidha, makampuni ya bima pia yameondoa dawa kadhaa, hasa za moyo, katika orodha ya matibabu yaliyorejeshwa, na kuwaacha wagonjwa kulipa bei kamili. Madaktari wa Iran wamebaini kuwa hali hii inahatarisha kuwakatisha tamaa watu ambao hawana uwezo wa kumudu dawa kuendelea na matibabu: “Wagonjwa wa saratani ambao dawa zao ni ghali sana wanaweza kuishia kujiuliza kwa nini wanatumia pesa nyingi bila hata kuwa na uhakika wa matokeo na kuacha matibabu yao,” ana wasiwasi Dk Reza.