Iran: Uingereza inashiriki katika mauaji Gaza kwa kukana mauaji ya kimbari ya Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ameikosoa Uingereza kwa kukanusha mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza, akisema msimamo huo wa “kuudhi” unaifanya London kuwa mshiriki katika jinai zinazofanywa na utawala wa Israel.

Baghaei alisema hayo katika ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti yake rasmi ya X, siku chache baada ya kamati ya Umoja wa Mataifa kusema kuwa vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza vina sifa za mauaji ya kimbari.

Katika ripoti iliyochapishwa Novemba 14, Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Mienendo ya Israel pia iliulaumu utawala wa Tel Aviv kwa “kutumia njaa kama silaha ya vita,” ambayo imesababisha “maafa makubwa ya raia na hali ya kutishia kwa maisha” Wapalestina.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, matokeo ya Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa yanayosema kwamba vita vya Israel dhidi ya Gaza vina sifa za mauaji ya kimbari ni sisitizo la yale ambayo tayari yamesemwa mara kwa mara na maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa kama Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa kuhusu Palestina, na maonyo ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

“Jambo jipya ni kwamba Uingereza inakanusha kidhalimu mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza,” amesema Esmaeil Baghaei na kuandika kwamba, idadi ya watu waliouawa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023, imefikia 43,846, na majeruhi ni 103,740.

Baghaei amesisitiza kwamba, matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy ya kukanusha kwamba Wapalestina wanakabiliwa na mauaji ya kimbari huko Gaza “yanalingana tu na sera ya serikali yake ya kuendelea kutoa silaha za mauaji na uungaji mkono wa kisiasa kwa utawala wa kibaguzi wa Israel, ambako kunaifanya Uingereza kuwa mshirika katika mauaji hayo kutokana na kikiuka majukumu ya kimataifa yaliyoainishwa katika Mkataba wa Mauaji ya Kimbari.”

Hivi majuzi, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu amekosoa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza na kusema kwamba anakanusha kutokea jinai hiyo katika eneo hilo la Palestina.

Francesca Albanese  amemtaja Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy kuwa “mkanushaji wa mauaji ya kimbari” na kusema kwamba Uingereza haijafanya “chochote” kuzuia ukatili huko Gaza.