Iran: Tutaendeleza jitihada za kidiplomasia hadi Israel ikomeshe jinai zake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, ataendelea kutembelea miji mikuu ya nchi mbalimbali na kuzungumza na viongozi wa nchi hizo hadi amani na utulivu upatikane katika eneo lote la Asia Magharibi.

Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo mara baada ya kuwasili Muscat, mji mkuu wa Oman akitokea Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumanne kwamba, ikiwa ni kuendelea na awamu ya tatu ya kuzitembelea nchi mbalimbali za ukanda huu, ameamua kuelekea Oman na kuonana na waziri mwenzake wa nchi hiyo Sayyid Badr bin Hamad Al Busaidi na kubadilishana naye mawazo kuhusu masuala ya pande mbili, ya kieneo na kimataifa.

Uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mzuri sana tangu zamani. Hapa ni wakati rais wa zamani wa Iran alipofanya mazungumzo ya simu na Sultan wa Oman

Amefafanua zaidi kwa kusema, katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, ametilia mkazo wajibu wa kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano mzuri, wa jadi, wa kidugu na wa kupendana baina ya Tehran na Muscat na wajibu wa kuendelea kushirikiana katika utatuzi wa migogoro ya eneo hili. 

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, Sayyid Abbas Araghchi, ameshafanya awamu tatu ya safari za kutembelea nchi mbalimbali za eneo hili huku ajenda kuu ikiwa ni kukomesha jinai za Israel huko Palestina na Lebanon na kukabiliana na njama za utawala wa Kizayuni za kutaka kuzusha vita vikubwa katika ukanda huu mzima.